WEKUNDU wa Msimbazi Simba wamefanikiwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili kiungo mshambuliaji, Peter Mwalyanzi kutokea Mbeya City fc.
Mwalyanzi alisaini mkataba huo jana na baada ya hapo alifanya mahojiano maalumu na Sports Xtra ya Clouds fm na hapa chini ni baadhi ya mambo aliyozungumza:
Swali: Kabla hujawa Peter Mwalyanzi wa leo, ulianza kucheza mpira wapi?
Mwalyanzi anaeleza: “Nilianza kucheza mpira nikiwa shule, nilikuwa napenda sana mpira. Nilipomaliza kidato cha nne nikasajiliwa Kijiweni ya Mbeya, baadaye ikaja kuuzwa na kubadilishwa jina kuwa TMK. Minziro (Fred) alikuja Mbeya, kuna baadhi ya wachezaji ikabidi waondoke na ile timu, hawakutakiwa kuondoka watu wote, wakachagua watano na mimi nikiwemo.
Tulicheza TMK, lakini hatukufanikiwa kupanda ligi kuu, wakapanda Manyema , Africa Lyon na Majimaji, ambao tulikuwa tunacheza 9 bora pale uwanja wa Uhuru .
Wale wachezaji watano Mtemvu (Abass), wote alikuwa anatukalisha Gesti, kwahiyo ikawa gharama, kwake na ikabidi wachujwe, nikabaki peke yangu TMK. Nilipoona ile timu haiangalii mbele zaidi, nikasajili Pan Africa wakati huo kocha akiwa Juma Pondamali ‘Meansah’.
Kipindi ambacho tulikuwa tunacheza tisa bora, tulikuwa na Mgambo JKT kabla ya kupanda ligi kuu. Waliniona na kuniita Tanga, hatimaye nikasajili pale.
Swali: Baada ya kusajiliwa Mgambo, msimu wako wa kwanza wa ligi kuu soka Tanzania bara ulikuwaje?
Mwalyanzi anaeleza: “Msimu wangu wa kwanza haukuwa mzuri pale Mgambo, mechi nne za kwanza zilikuwa ngumu kwangu, mwalimu alikuwa hanielewi kwasababu mpira wangu ulikuwa laini.
Alikuja kunipa nafasi kwenye mechi na Mtibwa Sugar, nikamuonesha kwamba alivyokuwa ananifikiria sivyo, baada ya mechi hiyo, Mgambo wakawa wananihitaji kuwepo uwanjani kila mechi. Nilicheza misimu miwili Mgambo.
Swali: Baada ya kucheza misimu miwili Mgambo, zilitoka taarifa za Yanga na Simba kukuwinda, ilikuwaje?
Mwalyanzi: “Nilipomaliza msimu wa pili pale Mgambo, Yanga wakawa wananihitaji, nikaja mpaka huku Dar es salaam, nikafanya nao mazungumzo, lakini viongozi wakagawanyika, baadhi walikuwa wananitaka mimi wengine wanamtaka Hassan Dilunga, wakaonekana wa Dilunga wameshinda, Bin Kleb akaniambia wewe nenda tutakupigia Simu.
Swali: Baada ya Yanga kuachana na wewe, ulikwenda wapi?
Mwalyanzi: “Nikaenda Mbeya na kukaa huko. Prisons wakanipigia simu, tukakubaliana kila kitu, nikawaambia mimi nimemaliza ligi sasa hivi, sio ninyi pekee mlioniona, kuna timu nyingine kama Mtibwa, Coastal, zote zimenipigia simu. Fanyeni haraka ili tumalize hii shughuli, wakasema sawa, lakini wao Mbeya sio makao makuu, inabidi wapate pesa kutoka Dar es salaam.
Nikakaa siku mbili, viongozi wa Mbeya City wakanipigia Simu, tukaongea nao na wakawa haraka, tukamalizana kila kitu, nikasaini mkataba kuitumikia msimu uliokwisha mei 9 mwaka huu.
Swali: Kabla ya kutakiwa na Simba, ulipata ofa ngapi hapa katikati?
Mwalyanzi: Hapa katikati kabla ya kuja Simba nimepata ofa mbili kutoka Mwadui na Yanga. Watu wa kwanza kuwasiliana na mimi walikuwa Yanga. Ile mechi ya mwisho dhidi ya Polisi sikucheza kwasababu nilikuwa na majeruhi, siku hiyo akanipigia simu kiongozi wa Yanga, Aron Nyanda wakati timu yao inacheza mechi Mtwara, akaniambia kocha amesema anakutaka wewe Peter Mwalyanzi ili uchukue nafasi ya Mrisho (Ngassa) kwasababu una kasi inayofanana na yake.
Nikawa nawasiliana na Aron, lakini akawa hanielezi kwa ufasaha, anaongea na mimi kama mdogo wake tu. Nikawa namsikiliza tu, kuna siku nikamtumia meseji nikimuuliza ‘Broo’ mboni kimya? Siku ya pili yake akanipigia simu, lakini sikuipokea kwasababu nilikuwa nje. Siku ya pili viongozi wa Simba wakanipigia simu, nikawa naongea nao kwa makini na jamaa alionekana yuko makini, akaniambia Simba tunakuhitaji si kwababu umetufunga mechi ya Mbeya, tumekufuatilia kwa muda mrefu.
Swali: Vita ya Simba na Yanga ilikuwaje siku mbili kabla ya kusaini Msimbazi?
Mwalyanzi: Jana (juzi) niliendea kuangalia mpira pale Mwenge-Mbeya, kuna watu wakaniambia utapigiwa simu na kutumiwa tiketi uende Dar. Mimi sikujua kitu na sikutaka kuuliza. Nikiwa pale Mwenge-Mbeya akanipigia simu kiongozi mmoja akiniambia mpango huo, lakini awali nilikuwa na mpango wa kuja Dar kwa ndege, kuna binamu yangu anafanya kazi Fastjet, alikuwa amenikatia tiketi achana na ya Simba waliotaka kukata.
Nikamwambia kiongozi wa Simba nakuja Dar jumapili, lakini sijui ni saa ngapi kwasababu hiyo tiketi natumiwa kwenye e-mail, akaona kama namdanganya hivi. Akaniambia kwani hiyo tiketi vipi? Sisi tunakukatia nyingine, nikawaambia sasa hiyo nyingine itakuwaje? Akaniambia usijali, akanitumia tiketi nyingine, nikamwambia binamu aachane na kunitumia tiketi.
Yule kiongozi wa Simba akawa ananipigia simu mara kwa mara akisema bwana nimesikia Yanga wanakutumia tiketi uje, nikamwambia mimi sijui. Kila muda ananipigia bwana usirubunike, tunakuomba sana. Nikamwambia mimi nikikwambia kitu nitafanya basi nitafanya, siwezi kurubunika kwasababu ya kitu fulani.
Juzi asubuhi saa 12 kanipigia simu mtu mmoja akiniuliza, vipi uko wapi? Nikamwambia nipo home, akasema uko home wapi wakati uko Airpot hapo (Mbeya)? Nikamwambia naenda Dar kuonana na Mtibwa sio huko unakosema wewe. Kweli nikasafiri na kukutana na wale jamaa wa Simba. Jinsi walivyokaa huwezi kujua kama wanamsubiria fulani, mmoja kakaa huku, mwingine kakaa kule. Kuna broo nilikuwa namjua pale, nikaenda alipo, akanichukua tukaenda mpaka kwenye gari, hatimaye tukaenda ofsini, tukakubaliana mahitaji ya msingi, tukaafikiana kwa pande zote mbili na nikasaini mkataba wa miaka miwili nikiwa na ndugu yangu anayejua sheria.