AZAM FC imelazimishwa sare ya
kufungana bao 1-1 na African Sports
ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara usiku huu
Uwanja wa Azam Complex, Chamazi,
Dar es Salaam.
Sare hiyo inaiongezea Azam FC pointi
moja na kufikisha 36 baada ya mechi
14, ikiwazidi pointi tatu mabingwa
watetezi, Yanga SC walio katika
nafasi ya pili, ingawa wana mechi
moja mkononi.
Katika mchezo uliochezeshwa na refa
Jonesia Rukyaa wa Kagera
aliyesaidiwa na Ferdinand Chacha na
Julius Kasitu, hadi mapumziko Azam
FC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na kiungo wa
zamani wa Yanga SC, Frank Raymond
Domayo dakika ya 28 kwa shuti la
umbali wa takriban mita 20, baada ya
kupokea pasi ya Nahodha John
Raphael Bocco.
Pamoja na kumaliza dakika 45 za
kwanza, wakiwa nyuma, lakini African
Sports walionyesha upinzani kwa
Azam FC na mara mbili walikaribia
kupata bao.
Kipindi cha pili, Sports iliyo chini ya
kocha wa zamani wa Simba SC,
Ramadhani Aluko iliongeza bidii na
kufanikiwa kusawazisha bao hilo
dakika ya 59 kupitia kwa Hamad
Mbumba aliyemalizia mpira wa
adhabu uliopigwa na Mwaita Gereza.
Baada ya bao hilo, timu hizo
ziliendelea kushambuliana kwa zamu
na kosakosa zilikuwa za pande zote
mbili.
Matokeo hayo yanaipunguza kasi
Azam FC katika mbio za ubingwa na
sasa, mabingwa watetezi, Yanga SC
wanaweza kurejea kileleni iwapo
watashinda dhidi ya Ndanda FC
kesho.
Kwa African Sports, sare hiyo ya
ugenini inakuwa ahueni katika
harakati zao za kujiepusha na balaa la
kushuka daraja.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi
Manula, Shomary Kapombe, Waziri
Salum/Farid Mussa dk62, Abdallah
Kheri, Serge Wawa, Erasto Nyoni,
Jean Baptiste Mugiraneza, Salum
Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco
‘Adebayor’, Frank Domayo/Mudathir
Yahya dk65 na Kipre Herman
Tchetche.
African Sports; Zakaria Mwaluko,
Mwaita Gereza, Khalifa tweve, Rahim
Juma, Juma Shemvuni, Ally
Ramadhani/James Mendi dk86,
Mussa Chambega, Pera Ramadhani,
Hamad Nathaniel, Hassan Materema/
Mohammed Mtindi dk47 na Rajab
Isihaka/Hussein Issa dk70.