Goran Kopunovic
UONGOZI wa Simba umethibitisha
rasmi kuachana na aliyekuwa kocha mkuu wake, Mserbia Goran Kopunovic
baada ya kushindwa kufikia makubaliano juu ya mkataba mpya.
Mwenyekiti wa kamati ya usajili
ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema Kopunovic ameshuka kidogo mno
kwenye dau alilotaka na Simba wameshindwa kufikia uwezo huo.
“Amebaki palepale, ameshuka
kidogo sana, tumeona atafute maslahi ya namna hiyo kwenye timu nyingine,
sisi hatuwezi kufikia. Unaweza kusema hakushuka kabisa, yaani katika
hela zote alizotaja ameshuka kwa dola elfu tano tu”. Amesema Hans Poppe
na kuongeza: “Tumeshaona makocha karibu sita kutoka Serbia, Hungary,
Bulgaria na Burundi pia tunaangalia, kuna kocha ambaye CV zake ni
nzuri”.
Goran Kopunovic
Hans Poppe ameongeza: “Hatudaiani
na Kopunovic, mkataba wake umekwisha. Mrithi wa Goran ndani ya wiki
moja tutakuwa tumempata. Atakakuja kocha tu, wasaidizi wataendelea
walewale, hatukupenda kubadilisha, lakini bahati mbaya tumeshindwa
kuafikiana, amekwenda juu mno tofauti na matarajio yetu, tungependa
kuendelea na Kopunovic, ni kocha mzuri, ameifundisha timu vizuri”.
Kopunovic alitaka mshahara mkubwa wa dola za Kimarekani elfu tisa (9,000) sawa na shiloingi milioni 18 za Kitanzania.
Pia anataka dau la kusaini la dola za kimarekani elfu hamsini (50,000) sawa na shilingi million 100 za Kitanzania.
Taarifa zilizoripotiwa jana ni
kwamba kocha Mbelgiji, Piet de Mol atatua Dar es Salaam Mei 21, mwaka
huu kwa ajili ya mazungumzo ya kuifundisha Simba SC.
Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia,
De Mol mwenye umri wa miaka 60 ana uzoefu mkubwa wa kufundisha soka
Afrika, Asia na Ulaya na alikuwa nchini Ghana akifanya kazi ya
Mkurugenzi wa Ufundi wa akademi mjini Kumasi. Pia alifanya kazi na
Asante Kotoko. Pia alifundisha timu ya kwao Ubelgiji, Dubai, Qatar na
China. Alikuwa kocha Msaidizi wa AA Gent kuanzia mwaka 1997 hadi 2001.
Naye kopunovic leo akiwa
Hungary amethibitisha kushindwana na Simba, lakini amedai kuwa atakuwa
shabiki mkubwa wa timu hiyo kwani hakupenda kuondoka.
Simba imekosa kushiriki michuano ya kimataifa kwa miaka mitatu, kwa mara ya mwisho ni mwaka 2012 walipotwaa ubingwa wa Tanzania.
Moja ya sababu kubwa Simba kuchemsha katika michuano ya ligi kuu ni mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha.
Toka walipochukua ubingwa
2011/2012 chini ya kocha Maserbia Milovan Circovic, Simba imepitia
mikononi mwa Mfaransa Patrick Liewig, Mzawa Abdallah Kibadeni, Mcroatia,
Zdravko Logarusic, Mzambia Patrick Phiri na sasa wameachana na Mserbia,
Goran Kopunovic.
0 maoni:
Post a Comment