Na Haji balou
Klabu ya Simba imeweka msisitizo kwamba mechi ya Jumamosi dhidi ya Coastal Union ni ya mwisho kwao hawatacheza tena hadi Yanga na Azam FC wacheze mechi zao za viporo.
Simba itakuwa Tanga Jumamosi kuivaa Coastal Union katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Mkuu wa kitengo cha habari cha Simba, Haji Manara ambaye jana alilizungumza hilo, leo amesisitiza kwamba watakuwa na msimamo huo kwa sababu kuu tatu.
“Moja, hakuna sababu ya timu nyingine kuwa na viporo hata baada ya kucheza mechi za kimataifa,” alisema Manara.
“Mbili, hakukuwa na sababu Yanga isicheze Jumatano. Baada ya sisi kucheza Tanga wao watakuwa na viporo vitatu, unafikiri tunaweza kumaliza ligi kugombea ubingwa kwa timu nyingine kuwa na michezo mitatu mkononi. Umewahi kuona kwenye ligi ipi makini duniani?”
“Tatu, kama zitabaki na viporo vitatu, timu nyingine zimeishacheza. Maana yake zipo ambazo zitakuwa zimeteremka daraja. Ushindani utakuwa hakuna tena, wakikutana nazo inakuwa ni rahisi sana kwao kushinda.”
Simba ndiyo ipo kileleni ikiwa na pointi 54, wakati Yanga na Azam FC ziko katika nafasi ya pili na tatu, kila moja ikiwa na pointi 50 na kila moja ina mechi mbili mkononi.
0 maoni:
Post a Comment