Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Baada ya kuwachapa ‘Makhrikhri’ BDF XI FC ya Botswana, kikosi cha Yanga SC tayari kimo jijini Mbeya kusaka pointi sita za Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya kuwafuata maafande wa BDF XI FC mjini Gaborone, Botswana.
Baada ya kuwachapa ‘Makhrikhri’ BDF XI FC ya Botswana, kikosi cha Yanga SC tayari kimo jijini Mbeya kusaka pointi sita za Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya kuwafuata maafande wa BDF XI FC mjini Gaborone, Botswana.
Wakiwa jijini Mbeya jioni hiui, Yanga SC wametamba kuchukua pointi zote sita katika mechi mbili za Ligi Kuu jijini humo dhidi ya timu ‘kibonde msimu huu’, Tanzania Prisons na Mbeya City FC.
Jerry Muro, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, ameuambia mtandao huu muda mfupi uliopita kuwa wachezaji wametua jijini Mbeya salama wakitokea jijini hapa.
Muro, mwandishi bora wa habari nchini miaka minne iliyopita, wachezaji wametinga jijini Mbeya kwa mafungu, baadhi wakisafiri kwa ndege na wasiopenda usafiri huo wa anga wamesafirishwa kwa basi.
“Tumeingia Mbeya kwa malengo mawili; kwanza kuchukua pointi zote sita katika mechi mbili zijazo dhidi ya Prisons na Mbeya City ili tukae vizuri katika msimamo wa Ligi Kuu. Pili, kufanya maandalizi ya mechi ya marudiano na BDF XI FC nchini Botswana,” amesema Muro.
Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Alhamisi Yanga SC itashuka Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya kuwakabili Prisons kabla ya kuchuana na wababe wa Simba SC, Mbeya City FC kwenye uwanja huo Jumapili.
Baada ya mechi dhidi ya City FC, Yanga SC wataanza safari kuelekea mjini Gaborone, Botswana kwa ajili ya mechi yao ya marudiano dhidi ya ‘Makhrikhri’ BDF XI FC ya hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika Februari 27.
Kikosi cha Mdachi Hans van der Pluijm cha Yanga SC kiliinyuka timu hiyo ya Jeshi la Ulinzi la Botswana mabao 2-0 katika mechi ya kwanza Uwanja wa Taifa jijini hapa juzi (Jumamosi).
Shukrani kwa mabao ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, Mrundi Amisi Tambwe, yote akiyafunga kwa vichwa na kufikisha mabao manne katika mashindano yote msimu huu.
Wachezaji wawili, kiungo Nizar Khalfan na beki wa kati Pato Ngonyani, ambao wamebaki jijini hapa kutokana na maradhi.
Yanga SC kwa sasa inakamata nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 25, sawa na mabingwa Azam FC ambao wako kileleni mwa msimamo kwa faida ya tofauti nzuri ya mabao ya kutupia na kufungwa.
Azam FC inayonolewa na Mcameroon Joseph Omog, imefunga mabao 22 na kufungwa 12 wakati Yanga SC imetikisa nyavu za wapinzani mara 15 huku safu yake ya ulinzi inayoongozwa na Nahodha, Mzanzibar Nadir ‘Cannavaro’ imeruhusu mabao saba.
0 maoni:
Post a Comment