Mar 21, 2015

NGASSA APATA ‘GONJWA LA AJABU’ YANGA SC NA LEO HAWEZI KUCHEZA DHIDI YA MGAMBO

Na Mahmoud Zubeiry, TANGA
KIUNGO mshambuliaji wa Yanga SC, Mrisho Khalfan Ngassa amepata ugonjwa ambao yeye mwenyewe hauelewi na leo anaweza kukosa mechi dhidi ya Mgambo Shooting.
Yanga SC wanacheza na JKT Mgambo leo Uwanja wa Mkwakwani, Tanga katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, lakini Ngassa ambaye ni tegemeo kweli la timu hiyo hali yake tete.
Ngassa amesema kwamba alimaliza vizuri mechi dhidi ya Kagera Sugar Jumatano, Yanga SC ikishinda 2-1, lakini Alhamisi mambo yakageuka.
Mrisho Ngassa ameumia 'kiajabu ajabu' na leo hatacheza dhidi ya Mgambo Shooting Uwanja wa Mkwakwani, Tanga

“Nilikuwa napanda basi jana kwa safari ya kuja Tanga, mguu ukaanza kuuma. Maumivu yakazidi nikiwa kwenye basi. Tulipofika nikamuambia dokta. Ameanza kuhangaika nao tangu hapo, lakini wapi, hali bado tete,”alisema Ngassa jana usiku.
“Nimejaribu kuweka barafu kupoza maumivu, lakini hali bado si nzuri na sijui tatizo ni nini,”amesema Ngassa.
Wazi Yanga SC kumkosa Ngassa leo dhidi ya Mgambo ni pigo kubwa, kwa sababu mchezaji huyo amekuwa chachu ya ushindi katika klabu hiyo.
Wakati Yanga SC itaingia kwenye mchezo wa leo na kumbukumbu ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Kagera, Mgambo nao katika mchezo uliopita waliifunga 2-0 mjini hapa.


0 maoni:

Post a Comment