Mar 16, 2015

NOOIJ AMUITA DIDA STARS JAPO HAJADAKA MIEZI MITATU YANGA

Na Baraka Kizuguto, MOROGORO
LICHA ya kwamba hajacheza mechi yoyote tangu Desemba 13, mwaka jana alipodaka Yanga SC ikifungwa mabao 2-0 na watani SImba SC katika mechi ya Nani Mtani Jembe, lakini kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ ameitwa Taifa Stars.
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mholanzi Mart Nooj, ametaja kikosi cha wachezaji 27 watakaoingia kambini kujiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Malawi utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Machi 29, 2015 na Dida yumo kikosini.
Tangu atunguliwe mabao mawili, Yanga ikilala 2-0 mbele ya Simba mechi ya Mtani Jembe, Dida amekuwa akimuangalia Ally Mustafa ‘Barthez’ akifanya kazi kwenye lango wana Jangwani hao.
Dida aliyeruka juu akiwa na wachezaji wenzake wa Taifa Stars. Ameitwa Stars japokuwa hajadaka tangu Desemba 13, mwaka jana 

Taifa Stars inayotarajia kucheza na The Flames mwishoni mwa mwezi huu, itaingia kambini machi 22 machi  katika hotel ya Tansoma kujiandaa na mchezo huo kabla ya kuelekea jijini Mwanza machi 24 kwa maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo.
Mbali na Dida, wachezaji wengine walioitwa ni makipa Aishi Manula na Mwadini Ali, wote wa Azam FC, wakati mabeki ni Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris (Azam FC), Mwinyi Haji (KMKM), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Oscar Joshua (Yanga), Abdi Banda na Hassan Isihaka (Simba SC).
Viungo ni Frank Domayo, Salum Abubakar, Amri Kiemba, Mcha Khamis (Azam FC), Hassan Dilunga (Yanga), Said Ndemla (Simba), Haroun Chanongo (Stand United).
Washambuliaji Mwinyi Kazimoto (Al Markhiry - Qatar), Simon Msuva, Mrisho Ngassa (Yanga), Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta (TP Mazembe - DRC), John Bocco (Azam FC), na Juma Luizio (Zesco United - Zambia)
Timu ya Taifa ya Malawi inatarajiwa kuwasili jijini Mwanza machi 27, 2015 ikiwa na kikosi kamili, wakiwemo wachezaji nane wanaocheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini, Msumbuji, Congo DR na Zimbambwe.
Malawi inashika nafasi ya 91 katika viwango vipya vya FIFA Duniani vilivyotolewa mwezi huu, huku Tanzania ikipanda kwa nafasi saba na kushika nafasi ya 100.

0 maoni:

Post a Comment