Mar 10, 2015

TFF WAFUTA MCHEZO WA YANGA NA JKT RUVU KESHO

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeipatia tahfifu Yanga SC baada ya kuifutia mchezo wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliokuwa uchezwe kesho dhidi ya JKT Ruvu ili kuipa wasaa mzuri wa kujiandaa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga SC watakuwa wenyeji wa Platinum FC Jumapili katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika Raundi ya Kwanza, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kikosi kizima cha timu hiyo kimeingia kambini leo katika hoteli ya Tansoma kwa maandalizi ya mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa timu hiyo.

Yanga SC iliitoa BDF XI ya Botswana katika Raundi ya Awali kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya kushinda 2-0 nyumbani na kufungwa 2-1 ugenini.
Mwishoni mwa wiki, Yanga SC ilipoteza mchezo wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mbele ya mahasimu wa jadi, Simba SC kwa kufungwa 1-0, hivyo kupunguza idadi ya pointi wanazowazidi mabingwa watetezi, Azam FC kutoka nne hadi moja (31-30). 
Ligi hiyo, inaendelea leo Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, wenyeji timu ya Polisi Morogoro watawakaribisha Ruvu Shooting kutoka Mlandizi mkoani Pwani.
Mchezo kati ya Azam FC dhidi ya Mgambo Shooting uliokuwa ufanyike kesho Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga sasa nao umesogezwa hadi Jumamosi.

0 maoni:

Post a Comment