May 29, 2015

AZAM FC YAAJIRI MAKOCHA KUTOKA UINGEREZA

stewart
*Watoka Arsenal, Southampton za Uingereza
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
‘Baada ya muda mrefu wa fununu, Azam wamekata kiu leo na kuanika makocha wao wapya wanaotoka Uingereza.’

HII KUFURU! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya jana uongozi wa Azam FC kumtangaza Muingereza Stewart John Hall kuwa kocha mkuu mpya akisaidia na makocha kutoka klabu kubwa za soka ulimwenguni ikiwamo Arsenal ya Ligi Kuu ya England (EPL).
Baada ya muda mrefu wa kusubiri kitakachojiri, uongozi wa Azam kupitia kwa msemaji wake, Jaffar Idd Maganga, leo umetangaza kumrejesha Hall na mabadiliko mengine makubwa katika benchi la ufundi.

Maganga amesema kuwa Hall aliyewahi kuinoa Azam FC na kuipa mafanikio makubwa ukiwamo ubingwa wa msimu wa 2013/14 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (ingawa aliishia mzunguko wa pili na kumpisha Mcameroon Joseph Omog), amepewa mkataba wa miaka miwili na atakuwa akisaidiwa na Mganda George ‘Best’ Nsimbe.

“Kuna ongezeko na punguzo katika benchi la ufundi na idara ya utawala na fedha kutokana na uamuzi uliofanywa na uongozi wa Azam FC leo (jana),” amesema.
Mark Philip raia wa Uingereza aliyewahi kufanya kazi katika klabu ya Bolton Wanderers ya Uingereza na kituo cha kulea vijana wenye vipaji (Academy) cha klabu ya Aston Villa ya Uingereza pia, anakuwa kocha wa makipa wa Azam akisaidiwa na mzawa Idd Abubakar.

Philip mwenye leseni A ya UEFA katika ukocha, amepewa mkataba wa miaka miwili na matajiri hao wa Tanzania.

Aidha, Mromania Mario Mariana ameajiriwa kuwa kocha wa timu ya vijana ya Azam na atasaidiwa na wazawa Dennis Kitambi (aliyekuwa kocha mkuu wa Ndanda FC msimu uliopita kabla ya kutimkia Azam) na Idd Cheche.

Mariana mwenye leseni ya UEFA Pro katika ukocha, pia atakuwa akiionoa timu ya Azam ya wakubwa akiwa kocha wa viungo (Physical Fitness).
Katika idara ya utawala na fedha uongozi wa Azam FC umemwajiri Muingereza mwingine, El Bankya kuwa meneja wa idara hiyo.

Muingereza huyo mwenye asili ya Uganda aliyewahi kufanya kazi katika klabu za Arsenal na Southampton za EPL, amepewa mkataba wa miaka miwili pia.
“Waajiriwa wote wapya wanatarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam Juni 8 na tutaanza rasmi kambi ya michuano ya Kombe la Kagame Juni 15 hapa Dar es Salaam,” amesema zaidi Maganga.

0 maoni:

Post a Comment