May 7, 2015

MOURINHO KUONGEZA MKATABA MPYA CHELSEA, ASEMA ATAKAA DARAJANI HADI ABRAMOVICH AAMUE

KOCHA wa Chelsea, Jose Mourinho (pichani juu) amekubali kuongeza Mkataba wa miaka miwili katika Mkataba wake wa sasa, taarifa za vyombo vya Habari Uingereza zimesema leo.
Mourinho, mwenye umri wa miaka 52, alirejea Chelsea mwaka 2013 kwa Mkataba wa miaka minne na msimu huu ameiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010 na Kombe la Ligi.
Mara ya kwanza alipokuwa kazini Stamford Bridge, kuanzia mwaka 2004 hadi 2007, alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu England mwaka 2005 na 2006, sambamba na mawili ya Kombe la Ligi na moja la FA.
Mourinho tayari ndiye kocha anayelipwa zaidi England, mshahara wa jumla ya Pauni Milioni 8.4 kwa mwaka na gazeti la The Sun la Uingereza limeripoti kwamba Mkataba mpya utafanya awe analipwa Pauni Milioni 10.5 kwa mwaka.
Akizungumza baada ya Chelsea kutwaa taji la Ligi Kuu ya England kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Crystal Palace Jumapili, Mourinho alisema atabaki katika klabu hiyo kwa muda mrefu atakaotaka Roman Abramovich, mmiliki wa klabu.
"Kama ambavyo nimekuwa nikisema tangu mwanzo wa msimu, nitabaki hapa kwa namna ambavyo Abramovich atataka mimi nibaki," amesema Mreno huyo. "Siku atakaponiambia ondoka, nitaondoka,”amesema.

0 maoni:

Post a Comment