Jan 15, 2016

FARIDI MUSSA APATA DILI CELTIC

WINGA wa kimataifa wa Tanzania,
Farid Malik Mussa anaweza kwenda
Celtic FC ya Ligi Kuu ya Scotland au
Athletic Bilbao ya Ligi Kuu ya
Hispania kwa majaribio.
Hiyo inafuatia wakala mmoja mwenye
mahusiano mazuri na klabu hizo
kuwasiliana na Azam FC, inayommiliki
Farid akisema Celtic na Bilbao ndizo
klabu ambazo zinahitaji mchezaji aina
ya Farid.
Na wakala huyo amefanikiwa
kuishawishi Azam FC iachane na ofa
ya wakala aliyekuwa anataka
kumpeleka Farid klabu ya FC Olimpija
Ljubljana ya Slovenia.
Taarifa ambazo BIN ZUBEIRY
SPORTS – ONLINE imezipata kutoka
Azam FC zinasema kwamba wakala
huyo anayetaka kumpeleka Farid
Celtic au Bilbao, tayari ametuma
fedha nchini ili mchezaji huyo apate
kozi za masomo ya lugha ya
Kiingereza.
Hata hivyo, mpango wa Slovenia
ulikuwa ni wa mapema zaidi kwa
Farid kwamba kama angekwenda
Hispania kukutana na klabu hiyo kwa
majaribio na kufuzu angesajiliwa
katika diridha hili dogo la Januari.

Lakini haijulikani mpango wa Celtic au
Bilbao kama unaweza kukamilika
katika dirisha hili la usajili au
baadaye.
Na Mtanzania ambaye aliwaunganisha
Azam FC na wakala wa timu ya
Slovenia anaamini klabu hiyo
inayomilikiwa na Alhaj Sheikh Said
Salim Awadh Bakhresa na familia
yake imegoma kumuuza mchezaji
huyo ili abaki kuwasaidia katika Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Ingawa, ndani ya Azam FC wanasema
wanachoangalia ni sehemu ambayo
Farid akienda atapata mafanikio zaidi,
lakini ukweli ni kwamba mchezaji
huyo kwa sasa yuko njia panda.
Baada ya kuzilinganisha ofa za
mawakala wote wawili, Azam FC
imevutiwa zaidi na yule ambaye
anataka kumpeleka Farid Celtic au
Bilbao.
Lakini kutokana na mipango ya Celtic
na Bilbao kuwa bado haijaiva, Farid
anaonekana kutamani aruhusiwe
aende FC Olimpija Ljubljana, ambako
tayari mwaliko upo mezani Azam FC.
Ikumbukwe Farid alitarajiwa kuondoka
wiki iliyopita kwenda Hispania
kuungana na klabu hiyo bingwa ya
Slovenia, FC Olimpija Ljubljana
iliyoweka kambi huko ambako alipewa
siku 10 za majaribio.
Mabingwa hao wa Slovenia waliweka
kambi nchini Hispania kujiandaa na
Ligi ya kwao na Farid alitarajiwa kuwa
nao kwa siku zote 10 akifanya nao
mazoezi kabla ya kuamua
kumununua.

0 maoni:

Post a Comment