KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC imeanza kwa sare katika harakati zake za kuwania ubingwa wa michuano maalumu nchini Zambia baada ya jioni ya leo kupata matokeo ya bao 1-1 dhidi ya wenyeji wao Zesco United ya huko.
Kocha wa Azam FC, Stewart Hall, aliingia kwenye mchezo huo kwa kukifanyia marekebisho matano
kikosi chake kwa kuwajumuisha mabeki David Mwantika, Pascal Wawa, Wazir Salum, kiungo
Frank Domayo na mshambuliaji Kipre Tchetche, ambao hawakucheza mchezo uliopita wa Kombe la FA dhidi ya African Lyon.
Mchezo huo uliathiriwa kwa kiasi kikubwa na mvua inayoendelea kunyesha jijini Ndola, Zambia,
baada ya Uwanja wa Levy Mwanawasa kusimamisha maji jambo ambalovlilifanya soka la
pasi kutotumiwa sana na timu hizo kufuatia mpira kunasa kwenye maji kila unapoburuzika.
Walikuwa ni Zesco United walioweza kuziona nyavu za Azam FC katika dakika ya kwanza tu ya mchezo huo, bao lililofungwa na mshambuliaji
mpya wa timu hiyo, Jesse Were, aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Kenya msimu uliopita akiwa na Tusker FC akifunga mabao 22.
Azam FC iliamka baada ya kufungwa bao hilo na kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa
Zesco United, lakini hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Wazambia hao waliondoka kifua mbele kwa bao hilo.
Kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kufanya mabadiliko akiingia kiungo Michael Bolou kuchukua nafasi ya Nahodha Msaidizi Himid Mao
'Ninja'. Mabadiliko hayo yaliweza kuisaidia sana Azam
FC baada ya kutawala kwa kiasi kikubwa eneo la
kiungo na kuanza kulishambulia kwa kasi lango la wapinzani wao.
Dakika 67 Azam FC ilipata pigo baada ya kuumia kwa nahodha wake John Bocco 'Adebayor' na
nafasi yake ilichukuliwa na Allan Wanga huku pia akitoka beki Wazir Salum na kuingia Ramadhan
Singano 'Messi'.
Kuingia kwa wawili hao kukizidi kuongeza kasi kwenye eneo la ushambuliaji la Azam FC na
katika dakika ya 70 beki Shomari Kapombe aliyeachiwa kitambaa cha unahodha na Bocco, almanusura aipatie bao la kusawazisha timu hiyo
baada ya kupiga shuti kali umbali ya mita 30 lililogonga mwamba wa juu na kutoka nje ya lango la Zesco United.
Azam FC ilizidi kuweka kambi katika lango la wapinzani wao dakika 15 za mwisho na hatimaye
ikajipatia bao safi la kusawazisha dakika ya 90 lililofungwa na Kipre Tchetche kwa kichwa
akimalizia kona safi iliyochongwa na Messi upande wa kulia.
Kona hiyo iliyozaa bao ilikuwa ni ya tatu kupigwa na Messi ndani ya dakika hiyo baada ya
wachezaji wa Zesco United kuokoa mara mbili za
mwanzo alizopiga kabla ya tatu haijazaa bao.
Hadi dakika 90 za mchezo huo wa kwanza
zinamalizika timu hizo zilitoka uwanjani zikiwa
nguvu sawa kwa mabao hayo.
Hiyo ni sare ya pili mfululizo baina ya timu hizo kwani katika michuano ya mwaka jana iliyofanyika jijini Lubumbashi DR Congo na
wenyeji TP Mazembe kuibuka mabingwa, zilitoka
sare ya mabao 2-2.
Azam FC itateremka tena dimbani Jumamosi Ijayo kucheza na mabingwa wa Zimbabwe
Chicken Inn kabla ya kumaliza michuano hiyo kwa kukipiga na Zanaco FC ya huko Jumatano
ijayo.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa hivi
Aishi Manula, Shomari Kapombe, Wazir Salum/
Ramadhan Singano 'Messi' dk67, Erasto Nyoni,
David Mwantika, Pascal Wawa, Jean Mugiraneza
'Migi', Himid Mao 'Ninja'/Michael Bolou dk46,
Frank Domayo 'Chumvi', John Bocco 'Adebayor'/
Allan Wanga dk67, Kipre Tchetche
0 maoni:
Post a Comment