KIUNGO wa Simba, Jonas Mkude,
ameonyesha masikitiko yake kwa mtindo
ulioanza kuzoeleka ndani ya Simba wa
ingia toka ya makocha kila uchao, akidai
inawavuruga, licha ya kwamba
wachezaji ni kama wanajeshi na katu
hawapaswi kuchagua pori la kupigania
vita.
Mkude alisema wachezaji wa Simba
wapo kwenye wakati mgumu, ingawa
jukumu lao ni kusimama imara ili kuona
timu yao inajenga heshima katika soka
la Bongo.
“Ukisikia utu uzima na kujielewa ndiyo
kipindi hiki ambacho tunakipitia
wachezaji wa Simba, kwani
kubadilishiwa makocha katikati ya
mechi ni mtihani kitu cha ziada ni kutoa
ushirikiano wa haraka kwa kocha
anayekabidhiwa kwetu kwa wakati
husika,” alisema.
Mkude alisema utakuwa msimu mgumu
kwao hasa wakiwa na nia ya kutimiza
kiu ya mashabiki wao wanaolilia
ubingwa. Lakini kwa kitendo cha
kuingia na kuondoka kwa makocha
kunawaumiza na kujikuta muda mwingi
wanatumia kuzoea makocha badala ya
kusonga mbele.
“Sisi tutakuwa tunafanya kazi ya
kuwakumbuka makocha wanapoondoka
na kuwazoea wanaoingia kama
binadamu inatugharimu, hata hivyo
tutapambana na tunaamini tutamzoea
Jackson Mayanja kama ambavyo
tuliwazoea makocha kina Patrick Phiri
na wenzake waliopishana Msimbazi,”
alisema. Mkude pia aliwataka
wanachama na kila mdau wa Msimbazi
kushirikiana pamoja ili kuivusha Simba
katika kipindi hiki ikiusaka ubingwa wa
Ligi Kuu baada ya kuukosa kwa misimu
mitatu iliyopita.
0 maoni:
Post a Comment