Mar 18, 2015

MANJI AMPANDISHA KIZIMBANI MFADHILI WA SIMBA, WAKILI NDUMBARO AIBUKIA MAHAKAMANI KUMTETEA

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
MFADHILI wa muda mrefu wa Simba SC, Muslah Al Rawah leo amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam kwa shitaka la kumjeruhi mtoto wa Mwenyekiti wa Yanga SC, Yussuf Manji, aitwaye Meheub Manji.
Wakili wa Serikali, Genis Tesha amesema wakati hati ya mashitaka kwambwa; Al  Rawah alifanya kosa hilo, Machi 8, 2015 kwenye Uwanja wa Taifa uliopo Chang'ombe .
Tesha amesema siku hiyo ya tukio, mshtakiwa Al Rawah alimpiga teke Meheub Manji na katika sehemu nyingine mbalimbali za mwili ukiwamo uso na kumsababishia majeraha mazito.
Muslah (kushoto) leo amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumpiga teke mtoto wa Manji

Al Rawah pia Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Simba SC, anayetetewa na Wakili Damas Daniel  Ndumbalo, alilikana shitaka hilo na upande wa mashtaka ukadai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika
Hata hivyo; baada kusomewa shtaka hilo, upande wa mashtaka uliiambia Mahakama kuwa hauna pingamizi na dhamana. Kwa upande wake, Wakili Ndumbalo naye aliomba mteja wake apewe dhamana.
Hakimu Frank Moshi akitoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa huyo, alimtaka awe na mdhamini mmoja ambaye anatoka katika taasisi inayotambulika Serikalini.
Baada ya mdhamini kujitokeza, upande wa mashtaka ulizifanyia uhakiki barua hizo ndani ya saa moja kama ilivyoelekezwa na Mahakama na mshtakiwa akaachiwa huru. 
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 20, 2015 kutoa nafasi upelelezi ukamilike.

0 maoni:

Post a Comment