Mar 18, 2015

SIMBA YAKALISHWA TANGA, YAPIGWA 2-0 NA MGAMBO, IVO ALIMWA NYEKUNDU, OKWI…

Na Princess Asia, TANGA
SIMBA SC imepunguzwa kasi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kufungwa mabao 2-0 na Mgambo Shooting Uwanja wa Mkwakwani, Tanga jioni ya leo.
Matokeo hayo yanazidi kuondoa matumaini ya Simba SC inayofundishwa na Mserbia, Goran Kopunovic siyo tu kutwaa ubingwa, bali hata kushika nafasi ya pili. 
Mgambo ilipata bao lake la kwanza kupitia kwa mchezaji wa zamani wa Coastal Union ya Tanga pia, Ally Nassor ‘Ufudu’ aliyemalizia krosi ya Fully Maganga.
Mapema dakika ya 21, Emmanuel Okwi aliikosesha Simba SC bao la wazi, baada ya kushindwa kuunganisha krosi nzuri ya Ibrahim Hajibu.  
Wachezaji wa Mgambo wakishangilia ushindi wao leo Uwanja wa Mkwakwani, Tanga

Dakika ya 35 pia, Okwi tena alishindwa kuunganisha krosi nzuri ya Hassan Kessy.
Kipindi cha pili ndipo jahazi la Simba lilipozama kabisa, baada ya kuongezwa bao la pili.
Bao hilo lilifungwa na Malimi Busungu kwa penalti dakika ya 66, baada ya kipa Ivo Mapunda kumchezea rafu Fully Mganga aliyekuwa anakwenda kufunga.
Emmanuel Okwi wa Simba SC akimizuia beki wa Mgambo, ili achukue mpira leo Uwanja wa Mkwakwani
Kiungo wa Simba SC, Abdi Banda (kushoto) akipambana na kiungo wa Mgambo 

Ivo alitolewa kwa kadi nyekundu na refa Amon Paul kutoka Mara, na Smba SC ikamuingiza kipa Peter Manyika kwenda kuchukua nafasi ya Said Ndemla. 
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda, Hassan Kessy, Mohammed ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murushid, Jonas Mkude, Abdi Banda, Said Ndemla/Peter Manyika dk66, Ibrahim Hajibu/Elias Maguri dk46, Emmanuel Okwi/Simon Sserunkuma dk79 na Ramadhani Singano ‘Messi’.
Mgambo Shooting; Godson Mmasa/Said Lubawa dk60, Bashiru Chanache, Salim Mlima, Salim Kipanga, Ramadhani Malima, Novaty Lufunga, Mohammed Samatta, Ally Nassor, Fully Maganga, Malima Busungu na Salim Aziz Gilla.

0 maoni:

Post a Comment