Apr 8, 2015

ILE ISHARA YA KUTULIZA, CHANONGO ASEMA ALIWATULIZA SIMBA


Kiungo mshambuliai wa timu ya Stand United, Haruna Chanongo, amewatuliza mashabiki wa Simba waliokuwa wakimzomea katika mchezo wa Stand United na Mtibwa Sugar baada ya kufanikiwa kuifungia timu yake bao pekee kwenye mchezo huo dhidi ya Mtibwa.

Mashabiki wengi wa Simba walikuwa jukwaani kwa kuwa kesho yake timu yao ilikuwa ikisubiri kupambana na Kagera Sugar.
Katika mchezo huo uliochezwa kwa siku mbili baada ya siku ya kwanza kuvunjika kutokana na mvua kubwa na kumalizika kesho yake, Chanongo alionyesha kiwango cha hali ya juu.
Hata hivyo, mashabiki hao ambao walikuwa wakizomea kila mchezaji huyo wa Simba aliyepelekwa Stand kwa mkopo alipogusa mpira, walinyamaza baada ya bao hilo.
Chanongo baada ya kufunga alikimbia kwenye jukwaani walilokaa na kuwaonyesha ishara ya mikono kuwa tulieni, hali iliyowafanya wawe wapole.
“Mimi sina ugomvi hata kidogo na Simba, nilishangaa kwa nini mashabiki wao walinizomea na kila mara nilikuwa nafikiria ni nini naweza kufanya ili niwatulize, nilipofunga ndiyo nikatumia ishara hiyo ya tulieni,” alisema Chanongo.

Aidha Chanongo amefafanua: “Mimi sijawakosea kitu mashabiki wa Simba lakini kitendo cha kunizomea kilinikosesha raha sana pale uwanjani na mimi nikajiuliza nifanye kitu gani ili waweze kunyamaza? Basi nilipofunga bao wakakaa kimya, hawakuzomea tena.”

0 maoni:

Post a Comment