Apr 8, 2015

TAMBWE APIGA NNE, SHERMAN AFUTA ‘MKOSI’ YANGA IKIUWA 8 - 0

Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
YANGA SC imezidi kujisogeza karibu na taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 8-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
Ushindi huo, unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 43, baada ya kucheza mechi 20- ikifuatiwa na Azam FC, ambayo baada ya sare ya 1-1 na Mbeya City leo, inafikisha pointi 37, baada ya mechi 19. 
Mshambuliaji Mliberia, Kpah Sean Sherman ‘amefuta mkosi’ leo, akifunga bao moja na kutoa pasi za mabao matatu- wakati Mrundi Amisi Tambwe amepiga ‘hat trick’.
Amisi Tambwe aliifungia Yanga SC bao la kwanza dakika ya tisa, akimalizia pasi ya Sherman, baada ya mpira wa adhabu uliopigwa na Oscar Joshua.
Amisi Tambwe amefunga manao manne Yanga ikishinda 8-0 leo dhidi ya Coastal Union Ligi Kuu 

Simon Msuva akaifungia Yanga SC bao la pili dakika ya 23 kwa shuti la mbali baada ya kupokea pasi ya Tambwe.
Dakika ya 34, Tambwe akaifungia Yanga SC bao la tatu akimalizia pasi ya Juma Abdul.  Tambwe tena akafunga bao lake la tatu katika mchezo wa leo na la nne kwa Yanga dakika ya 48, akimalizia pasi ya Sherman.
Sherman akaifungia Yanga SC bao la tano dakika ya 50 akimalizia pasi ya Tambwe. Mliberia huyo alimwaga machozi baada ya kufunga bao hilo na Mbuyu Twite akaenda kukipangusa kiatu chake kwa jezi yake. 
Msuva akaifungia Yanga SC bao la sita dakika ya 87 akimalizia pasi ya kichwa ya Tambwe. Msuva sasa ana mabao 13 katika Ligi Kuu akiwa anaongoza katika mbio za ufungaji bora, akifuatiwa na Didier kabumbangu wa Azam FC na Rashid Mandawa wa Kagera Sugar, wote wana mabao 10 kila moja.
Salum Telela akaifungia Yanga SC bao la saba dakika ya 88 kwa shuti kali akimalizia pasi ya Msuva, kabla ya Tambwe kufunga la nane dakika ya 90. 
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua/Edward Charles dk77, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mbuyu Twite/Hassan Dilunga dk67, Salum Telela, Haruna Niyonzima, Amisi Tambwe, Kpah Sherman/Nizar Khalfan dk70 na Simon Msuva.
Coastal Union; Bakari Fikirini, Juma Hamad, Abdallah Mfuko, Yussuf Chuma, Bakari Mtama, Abdulhalim Humud, Mohamed Ally, Yahya Ayoub, Rajab Mohamed/Mohammed Shekuwe dk57, Ike Bright Obinna/Mohamed Mtindi dk64 na Rama Salim/Abbas Athuman dk46. 
Sherman amefuta mkosi kwa kutoa pasi za mabao matatu na kufunga bao moja

0 maoni:

Post a Comment