WAKATI Azam fc wakidai idadi
ya wachezaji wa kigeni ligi kuu soka Tanzania bara iongezwe kutoka idadi
ya sasa ya watano, kocha wa Mbeya City fc, Juma Mwambusi amepinga
mtazamo huo.
Hoja ya Azam kutaka idadi
iongezeke ni kupata wachezaji wengi wa kigeni watakaowasaidia katika
michuano ya kimataifa pamoja na kuwapa changamoto wachezaji wazawa ndani
ya timu hiyo.
Makamu bingwa hao wa ligi kuu
msimu wa 2014/2015 wanadai wamejifunza kwa TP Mazembe na El Merreikh
ambao wamesheheni wanasoka wengi kutoka nje ya nchi zao.
Azam wakitoa hoja hizo, Mwambusi amesema haoni haja ya kuongeza wachezaji wa kigeni bali vipaji vya ndani viangaliwe zaidi.
“Siungi mkono kuongeza idadi ya
wachezaji wa kigeni katika soka letu la Tanzania kwasababu sisi tuna
wachezaji wengi wenye vipaji. Muhimu ni wachezaji wetu kujitambua
kwanza, halafu viongozi wa klabu zetu wanawachukuliaje wachezaji wetu?”
Amesema Mwambusi na koungeza: “Saa nyingine watu wanataka kusajili kwa
fasheni, vilabu vikubwa vinashindana kusajili wachezaji wa nje,
tusichukue wachezaji kwasababu tu tunataka kushindana na fulani,
tuwachukue wachezaji wa nje kwasababu wana kiwango cha juu ili waje
kuleta changamoto hapa kwetu”.
“Kwa idadi iliyopo inatosha
kwasababu tumeshaona hata hao watano kuna wengine wanakaa nje kwa
kushindwa na wazawa. Mimi nasema wachezaji wetu wanatakiwa kujitambua tu
ili wajue kuwa mpira ni kazi, wajitoe na kucheza kwa juhudi zote
uwanjani ili kuweza kuendeleza soka letu”.
“Wanaweza kuja hata wachezaji 11
wa kigeni, sijui kama itatusaidia, kikubwa tuangalie tulipojikwaa,
tusiangalie tulipoangukia. Viongozi wanaweza kusema vijana wetu
hawajitambui, sawa!, watajitambuaje? Kila mtu kwa nafasi yake katika
mpira afanye kazi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na kwa umakini
mkubwa, viongozi wanaotawala soka katika nchi yetu wana nia kweli ya
kuendeleza soka letu?. Tunaweza tukakubali kuleta wachezaji wengi,
lakini tusipopita kwenye mfumo sahihi hatuwezi kufika kokote”.
0 maoni:
Post a Comment