May 12, 2015

SIMBA SC YAMTUPIA VIRAGO DANI SSERUNKUMA, SIMON NA OWINO NAO…

Dani Sserunkuma ametupiwa virago Simba SC baada ya mechi 17 tangu Desemba aliposajiliwa kutoka Gor Mahia ya Kenya
Na Princess Asia, DARES SALAAM
MABINGWA wa zamani wa Tanzania na Afrika Mashafiki na Kati, Simba SC wamemtupia virago mfungaji bora wa zamani wa Ligi Kuu ya Kenya, Danny Sserunkuma baada ya makubaliano ya pande zote mbili jioni ya leo.
Mshambuliaji huyo raia wa Uganda aliandika katika ukurasa wake wa twitter jana saa 11:22 jioni akisema kuwa amefikia maamuzi ya kusitisha mkataba wa kuendelea kuichezea timu hiyo katika msimu ujao wa ligi bila kuweka wazi sababu zilizomsukuma kufanya hivyo.
Sserunkuma sasa atakuwa huru kujiunga na timu yoyote ambayo itamuhitaji kutumia kipaji chake.
"Simba na mimi (Sserunkuma) kupitia meneja wangu tumefikia maamuzi ya kuvunja mkataba kwa makubaliano yaliyoridhiwa na pande mbili hizi, tumesitisha ajira rasmi", ilisema kwa kifupi taarifa ya taarifa hiyo.
Katibu Mkuu wa Simba, Stephen Ally, amethibitisha kuwa ni kweli klabu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi imevunja mkataba na mganda huyo.
Ally alisema kuwa kufuatia maamuzi hayo, Sserunkuma sasa ni mchezaji huru na Simba haitamlipa kiasi chochote cha fedha.
Sserunkuma alisajiliwa na Simba mwezi Desemba mwaka jana akipewa mkataba wa miezi 12 ambayo ilikuwa inatarajiwa kumalizika mwaka huu.
Hadi anaondoka Simba SC, Sserunkuma aliyetokea Gor Mahia ya Kenya alikuwa amecheza mechi 17 na kuifungia mabao matano katika mashindano yote, matatu kati ya hayo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Bado wachezaji wengine wawili wa kigeni wamekalia kuti kavu ndani ya klabu hiyo iliyomaliza ya tatu katika msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ambao ni Simon Sserunkuma na Joseph Owino, wote Waganda.
Wachezaji wengine wa kigeni kikosini Simba SC ni Waganda pia, Juuko Murushid na Emmanuel Okwi waliokuwa wanakamilisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu.
Simba SC imemaliza katika nafasi ta tatu katika Ligi Kuu msimu huu, nyuma ya Azam FC waliokuwa wa pili na mahasimu, Yanga SC waliotwaa ubingwa.

0 maoni:

Post a Comment