BEKI wa Azam FC, Serge Wawa Pascal (pichani kushoto) amesema kwamba msimu wa kwanza aliutumia kujifunza kuhusu Ligi Kuu na soka ya Tanzania kwa ujumla, lakini msimu ujao ataanza kazi rasmi.
“Nimekuja hapa Desemba, kipindi chote nilikuwa najifunza kuhusu soka ya Tanzania na ligi ya hapa, naweza kusema hadi sasa nimekwishajua kiasi cha kutosha. Kwa hiyo kazi inaanza,”amesema.
Wawa aliyesajiliwa kutoka El Merreikh ya Sudan amesema kwamba awali alikuwa anafahamu ‘kijuu juu’ soka ya Tanzania, lakini sasa ameijua vizuri.
“Ligi ni ligi popote. Hakuna timu ya kudharau. Kila timu inapocheza na Azam inafanya bidii, hakuna mechi nyepesi kwa Azam,”amesema.
Beki huyo wa Ivory Coast amesema kwamba anaamini baada ya makosa waliyoyafanya msimu uliopita wakapoteza ubingwa, sasa wamejifunza.
“Tulipoteza ubingwa na kwa wachezaji maana yake tulipoteza fedha pia. Mnapopata taji, linaambatana na zawadi. Tumekosa. Naamini tumejifunza na msimu ujao hatutafanya makosa tena,”amesema.
Akiizungumzia michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati, Kombe la Kagame inayoanza wiki ijayo, Dar es Salaam, Wawa amesema kwamba ana uzoefu nayo na haimpi shida.
“Nimeshinda Kombe la Kagame mwaka jana nikiwa na El Merreikh. Ni michuano ambayo nina uzoefu nayo wa kutosha. Ni mizuri, ina changamoto nzuri,”amesema.
0 maoni:
Post a Comment