Jul 5, 2015

MKWASA: TIMU IMEBADILIKA, NIPENI MUDA NIWAPE RAHA ZAIDI

Na Baraka Kizuguto, KAMPALA
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars amesema wachezaji wake wamejitahidi kucheza vizuri hadi kupata sare ya ugenini na Uganda leo.
Stars imetupwa nje ya michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) baada ya sare ya 1-1 jioni ya leo Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda.
Matokeo hayo yanamaanisha, Stars imetolewa kwa kipigo cha jumla cha mabao 4-1, baada ya awali kufungwa 3-0 katika mchezo wa kwanza wa Raundi hiyo ya kwanza visiwani Zanzibar wiki mbili zilizopita.
Mkwasa kulia akiwa na Nahodha wa Stars, Nadir Haroub 'Cannavaro' 

Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya mchezo huo, Mkwasa amesema kwamba mchezo ulikuwa mzuri na timu yake ilitengeneza nafasi chache na kuweza kutumia moja.
Mkwasa alisema mechi hiyo ya kwanza Stars kucheza bila kufungwa baada ya kupoteza mechi tano mfululizo chini ya kocha aliyeondolewa, Mholanzi, Mart Nooij anaamini itarejesha amani katika timu.
“Ninawaomba Watanzania waendelee kutusapoti, tumekaa na timu kwa muda mfupi wa wiki moja tu, lakini katika mchezo wa leo mabadiliko yameonekana,”amesema.
Ameongeza kwamba wanahitaji muda kidogo kuweza kukaa na vijana kwa muda mrefu ili kujenga timu bora.
Stars inatarajiwa kurejea Tanzania siku ya jumatatu mchana kwa usafiri wa shirika la ndege la Rwanda Air.

0 maoni:

Post a Comment