Jul 16, 2015

SIRI YA DILUNGA KUSUSA YANGA SC HII HAPA…

Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
KIUNGO Hassan Dilunga (pichani) amegoma kuhudhuria mazoezi Yanga SC, kwa sababu ameambiwa atatolewa kwa mkopo Stand United.
Dilunga ameamua ‘kujifungia’ nyumbani kwao na kutokwenda mazoezini Yanga SC, huku uongozi wa klabu hiyo ukipanga kumchukulia hatua za kinidhamu.
BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE imeambiwa na rafiki wa karibu wa Dilunga kwamba ameamua kususa mazoezi kwa sababu haoni sababu ya kufanya mazoezi na timu ambayo hataichezea.
“Amegoma kwa sababu wamemuambia watamtoa kwa mkopo, naye amesema haoni sababu ya kufanya mazoezi na timu ambayo hataichezea,”amesema rafiki huyo wa Dilunga.
Mwenyewe Dilunga alikua mkali alipotafutwa na BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE na kusema hataki kuzungumza chochote kuhusu mambo yake na Yanga SC.
“Sitaki uandike chochote kutoka kwangu kuhusu mimi na Yanga SC, wewe iache kama ilivyo,”alisema jana Dilunga.
Yanga SC imeingia kambini jana katika hosteli za Chuo Cha Maaskofu, Kurasini mjini Dar es Salaam kujiandaa na michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Yanga SC ambayo imepangwa Kundi A pamoja na Gor Mahia ya Kenya, Telecom ya Djibout, KMKM ya Zanzibar na Khartoum-N ya Sudan, itakuwa ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini.
Mabingwa mara tano wa michuano hiyo, 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012, watafungua dimba na Gor Mahia Jumamosi jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mechi ambayo itatanguliwa na mchezo kati ya APR ya Rwanda dhidi ya Al Shandy ya Sudan Saa 8:00 mchana.

0 maoni:

Post a Comment