Haruna Niyonzima akiwa na mkewe leo Kigali, Rwanda baada ya kufunga ndoa ya Kiserikali |
UWEZEKANO wa kiungo Haruna Hakizimana Niyonzima kuichezea klabu yake, Yanga SC Jumamosi Dar es Salaam dhidi ya Azam FC ni mdogo.
Nahodha huyo wa Rwanda, amefunga ndoa na mkewe leo Kigali, baada ya kurejea kutoka Morocco kuichezea timu yake ya taifa.
Katibu wa Yanga SC, Dk. Jonas Tiboroha ameithibitishia BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE usiku huu kwamba, Niyonzima bado hajawasili.
“Niyonzima hajawasili, nadhani anaweza kuja kesho, kwa sababu walikuwa Morocco na timu yao ya taifa,”amesema Dk. Tiboroha.
Katibu huyo wa Yanga SC amesema mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe amewasili tangu juzi na leo amefanya mazoezi na wenzake Uwanja wa Boko Veterani, Dar es Salaam.
Yanga SC imeweka kambi hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani Pwani na inafanya mazoezi, uwanja wa Boko Veterani nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Azam FC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Aidha, kiungo Mnyarwanda wa Azam FC, Jean Baptiste Mugiraneza naye pia hajarejea Dar es Salaam, hivyo yuko hatarini kuikosa mechi hiyo ya kukata na shoka.
Niyonzima akiwatoka wachezaji wa Azam FC, Erasto Nyoni (kulia) na Khamis Mcha (kushoto) katika moja ya mechi zilizopita kuzikutanisha timu hizo |
0 maoni:
Post a Comment