Oct 16, 2015

SIMBA SC WAILAUMU TFF WAMEJAA NA UYANGA

Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
KLABU ya Simba SC imelalamika kwamba, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) haliwatendei haki kwa sababu uongozi wake umesheheni watu wa Yanga SC.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE leo kwamba, imefikia TFF wamekata kabisa mawasiliano na klabu yao.
Poppe amesema kwamba TFF sasa hawajibu hata barua za Simba SC wanapoandika kuhoji au kuomba ufafanuzi wa jambo lolote.
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amesema kwamba imefikia wakati wanashindwa hata kujua namna gani wanaweza kupata haki zao nyingine za msingi, kutokana na ‘kuchuniwa’ na TFF.
Hans Poppe amesema TFF haiwatendeo haki kwa sababu viongozi wengi ni Yanga SC 

“Inafahamika kwamba Rais wa TFF (Jamal Malinzi), Katibu wake (Mwesigwa Selestine) wote ni Makatibu wa zamani wa mahasimu wetu, Yanga SC. Na bado wapo wengine wengi pale TFF ambao wametoka Yanga akina Baraka Kizuguto.
“Lakini kwa sababu wanaongoza chombo cha kitaifa, wanapaswa kutenda haki, yaani inaonekana kabisa TFF wanaikandamiza Simba na wanaibebea Yanga,”amelalamika Poppe.
Akifafanua, mfanyabiashara huyo maarufu nchini, amesema TFF hawajajibu barua yoyote ya Simba SC kwa mwaka huu na hawaelewei sababu ni nini.
“Watuonyeshe wao, ni barya ipi ya Simba SC wamejibu mwaka huu, malalamiko yetu ya mchezo dhidi Yanga hawakujibu, Suala la Messi (Ramadhani Singano) hawakujibu. Hata tunapojibu barua zao za adhabu wanazotuandika ili kuomba ufafanuzi, pia hawatujibu. 
“Labda watuambie basi kwamba barua zetu tunatakiwa kuzipitishia Yanga SC ndiyo watujibu, tutafanya hivyo, tutaandika na kuwapelekea Yanga waweke muhuri wao ipelekwe TFF, tujibiwe, hiyo ndiyo shida yetu,”amesema.
Hans Poppe amesema kwamba mchezaji wao Ramadhani Singano ‘Messi’ amehamishiwa Azam FC kinyume cha utaratibu na kila wapodai haki yao hawasikilizwi. “Mchezaji wa Yanga (Donald Ngoma) alimpiga kichwa mchezaji wetu (Hassan Kessy) na tukapeleka ushahidi wa picha za video, hakuchukuliwa hatua na wala hatukujibiwa,”. 
“Lakini Juma Nyosso (wa Mbeya City) alimdhalilisha John Bocco (wa Azam FC) akachukuliwa hatua baada ya saa 24 kwa ushahidi wa picha,”amesema.
Aidha, amesema kwamba Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), limeiamuru klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia iilipe Simba SC dola 300,000 za Kimarekani za manunuzi ya mshmbauliaji Emmanuel Okwi, lakini wanashindwa kufuatulia kwa sababu TFF haiwasikilizi tena.
“Kwa kweli tupo wakati mgumu mno, tunashindwa hata kuelewa tunacheza hii ligi kwa sababu gani, inaonekana tunawasindikiza watu ambao tayairi wameandaliwa kwa namna yoyote wawe mabingwa,”amesema

0 maoni:

Post a Comment