Jan 16, 2016

KINACHOFANYA SAMATTA ACHELEWE KWENDA ULAYA NI HIKI HAPA

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
RAIS wa klabu ya Nantes ya
Ufaransa, Waldemar Kita
amesikitishwa mno na kitendo cha
mshambuliaji wa kimataifa wa
Tanzania, Mbwan Ally Samatta
kukataa ofa ya kujiunga na klabu
yake, lakini hajakata tamaa kwa
sababu kijana huyo bado ni mali ya
TP Mazembe.
“Tungependa kumpata.
Inavyoonekana amesaini (KRC Genk).
Lakini ni mali ya klabu gani? Atakuwa
huru mwishoni mwa msimu? Mawakili
wangu wanalishughulikia hilo suala
kwa siku mbili, au tatu,”.
“Kama itakuwa poa, au hapana, vizuri,
mbaya sana, yote maisha,” amesema
katika safu ya Ocean Press.
Wakati huo huo, tovuti ya Gazeti la
Lequipe la Ufaransa limeandika,
Samatta mwenye umri wa miaka 24
sasa, amekwishasaini Mkataba wa
awali na KRC Genk ya Ubelgiji.
Na lakini akiwa na Mkataba na TP
Mazembe hadi Aprili 30, Mwanasoka
huyo Bora Anayecheza Afrika hawezi
kuruhusiwa kwa dau la chini ya Euro
Milioni 1.
Na wakati Samatta tayari amepatiwa
viza na Ubalozi wa Ubelgiji kwenda
kusaini klabu ya KRC Genk, Rais wa
Mazembe, Moise Katumbi amegoma
kusikikiliza kuhusu klabu hiyo ya Ligi
Kuu ya Ubelgiji.
Rais wa Nantes ya Ufaransa,
Waldemar Kita amesikitishwa na
Samatta kukataa ofa ya kujiunga na
klabu yake
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE
inafahamu Katumbi anataka Samatta
aende Nantes FC ya Ligi Kuu ya
Ufaransa, ambayo amekwishafikia
makubaliano nayo.
Na wiki iliyopita Nantes FC ilituma
mwakilishi wake Dar es Salaam,
ambaye alifanya mazungumzo na
Meneja wa Samatta, Jamal Kisongo
mbele ya Ofisa mmoja wa Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF).
Katika mazungumzo, Kisongo alifikia
makubaliano ya maslahi binafsi na
Samatta ikiwemo dau la kusaini,
mshahara, masharti na marupurupu
mengine.
Kisongo alitaka kiwepo kipengele cha
mchezaji kutorejeshwa Afrika iwapo
hatapata nafasi ya kucheza Nantes,
bali auzwe klabu nyingine ya Ulaya na
ikakubaliwa.
Nantes ilionyesha nia ya dhati kabisa
ya kumchukua Samatta na Kisongo
aliinuka kwenye meza ya
mazungumzo akiwa amekubali na
kusema anakwenda kuzungumza na
mchezaji.
Hata hivyo, inaonekana Samatta
mwenyewe ndiye anayetaka kwenda
Ubelgiji na si Ufaransa, kwani kitendo
cha Kisongo kutorejesha majibu kwa
Nantes kinaashiria ameshindwa
kumshawishi mchezaji wake akubali
ofa hiyo.
Wakati huo huo, Rais wa Mazembe
hayuko tayari kumuuza Samatta
Ubelgiji na yuko tayari kuona Samatta
anabaki Mazembe kumalizia Mkataba
wake ili aondoke kama mchezaji huru
Aprili, hali ambayo itamlazimu kusubiri
hadi Agosti kusaini Genk.
Kwa sasa, kambi ya Samatta inajaribu
kuomba msaada kwa viongozi wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, wakazungumze na Katumbi
ili akubali kumuacha mchezaji aende
klabu aliyochagua.
Rais Mstaafu, Dk Jakaya Mrisho
Kikwete ambaye kwa sasa ni
Mwenyekiti wa chama tawala, CCM,
Waziri wa Michezo, Nape Nnauye kwa
pamoja wameahidi kumsaidia Samatta
katika suala la kumlainisha Katumbi
akubali kupokea ofa ya Genk.
Wakati huo huo, Nantes wamekuwa
wakimpigia simu Kisongo wakisema
wanamsubiri mchezaji aende kusaini,
lakini Meneja huyo anakosa majibu ya
uhakika.
Inaonekana tayari Katumbi anaujua
mchezo wote unaoendelea naye
ameamua kukaa kimya akiamini
Samatta hawezi kufanya chochote
kwa sasa bila baraka zake.
Na wazo la kusema Samatta asubuhi
hadi Aprili atakapomaliza Mkataba
wake ili asaini kama mchezaji huru
Agosti halifurahiwi hata na Kisongo
mwenyewe.
Samatta aliyejiunga na TPM mwaka
2011 akitokea Simba SC aliyoichezea
kwa nusu msimu, akitokea African
Lyon, hadi sasa ameichezea klabu
hiyo mechi 103 na kuifungia mabao
60.
Ndani ya mechi hizo, kijana huyo wa
umri wa miaka 24, ameshinda taji la
Ligi ya Mabingwa Afrika na Mazembe,
huku naye akiibuka mfungaji bora wa
michuano hiyo na kutwaa tuzo ya
Mchezaji Bora Anayecheza Afrika.

0 maoni:

Post a Comment