Feb 26, 2015

ALICHOSEMA KOCHA YANGA KUELEKEA MECHI YA KESHO BOTSWANA


pluijm
Na Bertha Lumala
Kocha mkuu wa Yanga SC, Hans van der Pluijm amewataka wachezaji wake kuhakikisha wanatikisa nyavu za wapinzani wao BDF XI FC katika mechi yao ya kesho ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Yanga SC, mabingwa mara 24 wa Tanzania Bara, watakuwa na kibarua kigumu mbele ya wenyeji wao hao watakapopamba katika mechi hiyo ya marudiano ya hatua ya awali ya michuano itakayochezwa kuanzia saa 2:00 usiku Uwanja wa SSKB Lobatse uliopo Km 70 kutoka Gaborone, mji mkuu wa Botswana. Uwanja huo upo kwenye kambi ya Jeshi la Ulinzi (BDF) eneo la Lobatse, Botswana.
Katika mahoajino na mtandao huu akiwa Botswana leo mchana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Jerry Muro amesema benchi lao la ufundi linaloongozwa na Pluijm limewataka wachezaji kuhakikisha wanapata japo goli moja la ugenini huku wakilinda mabao yao mawili waliyofunga nyumbani.
“Tulishinda 2-0 nyumbani, lakini kocha (Pluijm) amewataka wachezaji kutobweteka na ushindi huo. Amesema ni lazima tusakae japo goli moja la ugenini ili tuwe salama zaidi huku tukihakikisha wenyeji wetu hawapati mabao,” amesema Muro.
Pluijm amesema ushindi wa timu hiyo kwenye mechi za Ligi Kuu ni chachu kuelekea mchezo huo wa marudiano dhidi ya BDF
Aidha, mitandao ya michezo ya Botswana imemnukuu Pluijm akitamba kupata ushindi mwingine wakati timu hizo zitakaporudiana kesho.
Pluijm amekaririwa akieleza kuwa, licha ya kucheza ugenini, bado ana uhakika watawafunga wenyeji wao BDF XI FC katika mchezo huo.
“Tumekuja Botswana kucheza kwa kushambulia kama tulivyofanya nyumbani tuliposhinda mabao 2-0, ninajua mchezo utakuwa mgumu kwa sababu wanacheza kwao na watataka kutushambulia, lakini sisi tutacheza kwa malengo huku tukihitaji bao moja ili kuwapa presha wenyeji,” amesema Pluijm.
Pluijm amesema ushindi wa timu hiyo katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara ni chachu kuelekea mchezo huo wa marudiano dhidi ya BDF na kuwataka mashabiki kuiunga mkono timu yao kuelekea mechi hiyo.
Hata hivyo, mashabiki wa Yanga SC waliokuwa wasafiri kwa basi kubwa la klabu hiyo Jumatano alfariji, walikwama kutokana na kile kilichoripotiwa leo kuwa basi hilo halina bima wala kibali cha barabarani.
Yanga SC ambayo kwa muda mrefu imekuwa haifiki mbali katika michuano ya kimataifa ikitolewa kwa matuta dhidin ya Al Ahly ya Misri katika hatua ya pili mwaka jana, inahitaji sare ya aina yoyote au kipigo kisichozidi bao 1-0 kusonga mbele.
Endapo timu hiyo ya Jangwani ikifanikiwa kuwang’oa maafande hao, itakutana na mshindi kati ya Sofapaka FC ya Kenya na Platnum FC katika hatua inayofuata. Wazimbawe walishinda 2-1 dhidi ya Sofapaka katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Nairobi wiki mbili zilizopita.

0 maoni:

Post a Comment