Mar 17, 2015

SHERMAN AWAAMBIA YANGA WAMPE MUDA, WATAFURAHI NA ROHO ZAO

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
MSHAMBULIAJI Mliberia wa Yanga SC, Kpah Sean Sherman amewaomba mashabiki wa timu hiyo kumsapoti na kumpa muda, akiamini siku moja ataanza kuwafurahisha.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini Dar es Salaam, Sherman alisema kwamba anafahamu kiu ya mashabiki wa timu hiyo ni kumuona anafunga mabao na kuisaidia timu kufanya vizuri.
“Mimi ni mchezaji mzuri na ambaye najiamini. Mimi ni mshambuliaji halisi. Mimi ni mfungaji asilia. Bado sijaonyesha yote hayo hapa Yanga, lakini naamini wakati ukifika nitaonyesha,”alisema.
Kpah Sherman akiibusu nembo ya Yanga juzi kuashiria ana mapenzi na klabu hiyo
Sherman akiwapa ishara ya "Suala la muda" mashabiki wa Yanga juzi

Sherman alisema kwamba mwanzoni hali ya kukosa mabao ilimsababishia msongo wa mawazo hadi akajikuta anashindwa hata kucheza vizuri, lakini alipoamua kuikubali angalau anaanza kurudi kucheza katika kiwango chake.
Sherman alitokea benchi juzi katikati ya kipindi cha pili na kwenda kutoa pasi ya bao la tano, Yanga SC ikishinda 5-1 dhidi ya Platinum FC ya Zimbabwe katika mchezo wa kwanza, Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika.
Na baada ya kutoa pasi hiyo ya bao, lililofungwa na Mrisho Ngassa, Sherman alikimbilia mbele ya jukwaa la mashabiki wa Yanga na kubusu nembo ya timu, huku akionyesha ishara ya kugusa saa, kumaanisha “Ni suala la muda”.
Sherman ameiambia BIN ZUBEIRY;  “Kufunga mabao ni suala la muda tu, ukifika nitafunga tena sana, mashabiki wa Yanga lazima wajifunze kuwa na wachezaji wao. Wao wasiwakatishe tamaa wachezaji wao, hiyo kazi wawaachie Simba,”alisema.
Amesema yeye ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na hakuna shaka juu ya hilo, kikubwa anachoomba mashabiki wa Yanga wajenge imani juu yake na kumsapoti.
“Natakiwa nijivunie mashabiki wa timu yangu, wao wanatakiwa kunitia moyo. Wasinikatishe tamaa. Mimi nina uwezo, sibahatishi,”amesema mchezaji huyo aliyesajiliwa Desemba kutoka Cyprus alipokuwa anacheza soka ya kulipwa.  

0 maoni:

Post a Comment