Mar 2, 2015

YANGA SC KUKUTANA NA WAZIMBABWE KOMBE LA SHIRIKISHO


Na Vincent Malouda, ZVISHVAANE
VIGOGO wa ligi ya Tanzania bara, Yanga SC, watamenyana na klabu ya FC Platinum ya Zimbabwe katika raundi ya kwanza ya kombe la Shirikisho Afrika baada ya timu hiyo kuifumua Sofapaka FC ya Kenya na kusonga mbele kwa jumla ya magoli 4 – 2.
FC Platinum iliilaza Sofapaka 2 – 1 jana kwenye mechi ya mkondo wa pili iliyosakatwa alasiri ya leo katika uga wa Mandava mjini Zvishavane, Zimbabwe. Mshambulizi wa Sofapaka na Mburundi Fiston Abdoul Razak aliipa timu yake uongozi katika dakika ya nne lakini Wisdom Mtasa akazawazisha mambo baada ya robo saa.

Donald Ngoma wa Platinum (kushoto) amkimbiza Kevin Omondi wa Sofapaka

Timu zote zilipoteza nafasi za kuhesabika kabla ya refa wa katikati na Mbotswana Tirelo Mositwane kupuliza kipienga kuashiria mapumziko.
Katika kipindi cha lala salama, Mtasa alicheka na nyavu dakika ya 54 na kuua matumaini ya vijana wa kocha Mganda Sam Timbe kurejea mchezoni kwani walishindwa kufunga mabao manne ili kupenyeza awamu ijayo.
Platinum waliwazaba Sofapaka, maarufu kama Batoto ba Mungu 2 – 1 kwenye mkumbo wa kwanza uliyogaragazwa majuma mawili yaliyopita mjini Nairobi. Brian Muzondiwa na Donald Ngoma wakifunga katika mechi hiyo huku Fiston akisajili moja la kuvutia machozi.
Sofa sasa wanarejesha buti zao kutesa nyasi za nyumbani kwenye ligi kuu ya taifa, KPL, pindi tu mahakama itakaposikiza kesi iliyowasilishwa na kampuni inayosimamia ligi kuu kuhusu ombi la Shirikisho la Soka nchini, FKF, kusitisha ligi hiyo kuheshimiwa na kampuni hiyo ambapo hamna mechi zilizosakatwa katika ligi hiyo wikiendi hii.
Hayo yakijiri, ligi kuu ya FKF iliendelea siku ya jana mechi mbili zikipigwa katika viwanja tofauti. Bidco United iliwarambisha St. Joseph 3 – 0 sakafu katika uchanjaa wa Kaunti ya Thika, magoli ya Bidco yakifungwa na straika Hussein Puzzo, beki wa kushoto na mganda Patrick Senfuka na Simon Ng’ang’a dakika a 18, 54 na 78 mtawalia.
Katika uwanja wa Bukhungu mjini Kakamega, West Kenya iliandikisha ushindi wa 2 – 1 dhidi ya Kariobangi Sharks ya kutoka Nairobi. Peter Kihungi akiwazawidi West Kenya bao la kwanza kwa kujifunga kabla ya Johnson Indimuli na Rodgers Omondi kukamilisha mauaji.
Ligi hiyo inaendelea kesho Ligi Ndogo SC ikivaana na Modern Coast Rangers FC, FC Talanta na Finlays FC, zote ugani City, Nairobi. Zoo Kericho nyumbani baina ya Oserian FC kisha Agrochemicals FC ifunganye virago na Nairobi Stima kule Kisumu.

0 maoni:

Post a Comment