Apr 9, 2015

HANS POPPE: KESSY HAJITAMBUI WALA HAJIJUI

Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba beki Hassan Ramadhani Kessy hajatumia busara kususa wakati anaidai klabu hiyo Sh. Milioni 5, baada ya kulipwa Sh. Milioni 15 za usajili wake.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo Dar es Salaam, Poppe amesema kwamba walimsajili Kessy kwa dau la Sh. Milioni 20 Desemba mwaka jana na wakampa Sh. Milioni 15, wakiahidi kummalizia Milioni 5 baadaye.
Hata hivyo, Poppe amesema ni jambo la ajabu hata mwaka mmoja kati ya miaka miwili ya Mkataba wake haujamalizika, mchezaji huyo anagoma.
Amegoma; Hassan Kessy amejitoa kikosini Simba SC kwa sababu hajamaliziwa fedha za usajili na hajapatiwa nyumba ya kuishi
Amekoma naye; Zacharia Hans Poppe (kushoto) amesema hana hamu na mchezaji huyo chipukizi

“Huu ndiyo utaratibu wetu. Wachezaji wote tunaowasajili huwa hatuwapi malipo yote, mara nyingi tunawapa nusu, tunawamalizia baadaye. Tena yeye alikuwa ana bahati kupewa zaidi ya nusu,”.
“Na kuna wenzake wanadai fedha nyingi kuliko yeye, lakini hawajagoma. Kwa kweli huyu mchezaji si mfano bora na mimi amenikera sana. sina hamu naye,”amesema Poppe.
Aidha, Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba mshahara ambao Kessy anapata hivi sasa Simba SC ni zaidi ya mishahara sita aliyokuwa analipwa Mtibwa Sugar, lakini inashangaza bado anagoma.
“Kasajiliwa Desemba, kapewa Milioni 15 kati ya 20, kufika Machi anagoma, huyu mchezaji mzima kweli?”amehoji Poppe.
Hata hivyo, Poppe amesistiza suala la mchezaji huyo litapelekwa Kamati ya Nidhamu ya klabu na atachukuliwa hatua kwa sababu sheria ziko wazi.
Alipoulizwa kuhusu kutopatiwa nyumba, Poppe alijibu; “Klabu iliahidi kumpatia makazi, na hadi sasa bado tunahangaika kumtafutia makazi. Suala si makazi tu. Ni makazi bora na eneo salama. Sasa papara zake alitaka tumpeleke akaishi Tandale? Maana huko vyumba vinapatikana hata saa nane usiku,”. 
“Na kwa kawaida mchezaji anaposajiliwa Simba kabla ya kupatiwa nyumba, huwa anaishi hoteli na analipiwa na klabu. Huyu mtu ana matatizo tu yeye mwenyewe, asitake kuwachafua watu hapa,”amesema.  
Mbaya zaidi, Poppe amesema mchezaji huyo badala ya kupeleka malalamiko kwa uongozi, akakimbilia kwenye magazeti. “Ina maana lengo lake aipake matope klabu, basi kafanakikiwa,”amesema Poppe.

0 maoni:

Post a Comment