Apr 13, 2015

MSUVA SASA AMTAMBIA KAVUMBAGU, AMUAMBIA KIATU CHA DHAHABU MALI YAKE

Baada ya kumzidi kwa idadi ya mabao matatu, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva, amemwambia mshambuliaji wa kutegemewa wa Azam FC, Didier Kavumbagu asahau ufungaji bora kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Bara.


Msuva jana aliiongoza timu yake kuvaana na Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Msuva alisema kuwa, kamwe hatakubali kuona mshambuliaji huyo anampita kwenye mbio hizo za ufungaji bora.

Alisema kuwa, bado anaendelea kushika maelekezo na mafunzo anayoyapata kutoka kwa kocha wake Mholanzi, Hans van Der Pluijm na msaidizi wake Charles Mkwasa kuhakikisha anafunga na anawatengenezea wenzake nafasi za kufunga mabao.

“Sitaki kuondoka hapa nilipo katika orodha ya wafungaji bora, lengo kubwa likiwa ni kumaliza ligi kuu nikiwa mfungaji bora msimu huu, ninaamini hilo linawezekana kabisa.

“Hivyo, nitahakikisha ninaitumia vyema kila nafasi ninayoipata ndani ya uwanja kwa kufunga mabao ili niipe timu yangu ubingwa kwenye msimu huu na ufungaji bora.


“Ninafurahia ushirikiano mkubwa ninaoupata kutoka kwa wachezaji wangu katika kufanikisha malengo yangu kwa kunitengenezea nafasi nzuri za kufunga mabao,” alisema Msuva.

0 maoni:

Post a Comment