Feb 18, 2015

ANGALIA TAKWIMU ZA USHINDANI KATI YA RINALDO NA MESSI

Na Saleh Ally
KIUNGO Said Ndemla wa Simba na Simon Msuva wa Yanga ni kati ya Watanzania wanaofanya vizuri katika soka kipindi hiki.


Mwendo wao umekuwa mzuri ingawa si rahisi kujua kipimo chao ni nani hasa. Kwamba wanataka kumfikia au kushindana na nani wanayetaka kumpita.

Kushindana na mtu ni sahihi kwa lengo la kufanikiwa. 
Ushindani wa Cristiano Ronaldo wa Real Madrid na Lionel Messi wa Barcelona, uko wazi na hauhitaji mtu kuutafsiri au kutangaza.

Si rahisi kusema Ronaldo na Messi wanalala usingizi wa pono kutokana na ushindani mkubwa ulio mbele yao, ushindani binafsi, wa klabu na wa dunia nzima.

Wana kila kitu kwa maana ya kipato bora, lakini kila mmoja hana amani na ndiyo maana juhudi zao hazijawahi kukoma na leo huyu yuko juu, kesho mwingine.

Sasa Messi anaonekana kukwea kileleni kwa mambo kiufundi hali ambayo bila shaka inamfanya Ronaldo asiwe na amani au usingizi wa kutosha.

Hii inaonyesha ni kwa kiasi gani wachezaji wakubwa wenye uwezo wa juu ambavyo wamekuwa wakifanya kila linalowezekana ili kung’ara.

Ushindani wa Messi na Ronaldo, unawasaidia wote wawili lakini ni msaada mkubwa kwa Barcelona na Real Madrid kuendelea kufanya vizuri. Je, Msuva na Ndemla nao wana presha za namna hiyo?

Inawezekana ikawepo lakini kwa kiwango cha chini, lakini kama hakuna kabisa, basi ni tatizo maana yake ni sawa na mwenyewe kushindana na mwenyewe na haiwezi kuwa sawasawa na badala yake ushindani wa Messi na Ronaldo unaweza kuchukuliwa kama ushindani wenye shule hata hapa nyumbani Tanzania. 

Angalia takwimu zao na bado wanaendelea kuchukuana.
MABAO
Cristiano:
Amefunga mabao 36 katika mashindano yote. Kati ya hayo, 28 katika La Liga, matano Ligi ya Mabingwa Ulaya, Mawili mechi ya Super Cup na moja Copa del Rey.
Messi:
Ametupia mabao 37 katika mashindano yote. Mara  26 katika La Liga, nane katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na matatu Copa del Rey.
PASI ZA MWISHO
Cristiano:
Katika pasi zilizozaa mabao, Mreno huyo ametoa tisa kwa wenzake.
Messi:
Muargentina huyo ndiye anaongoza kwa pasi zilizozaa mabao, amegawa 12.

UMBALI
Cristiano:
Kila mmoja amekimbia kiasi cha juu uwanjani katika kila mechi aliyocheza. Ronaldo ameweza kukimbia kilomita 8.38 kwa mechi.
Messi:
Messi ana kasi zaidi uwanjani, pia ana uwezo wa kukimbia umbali mrefu katika mechi kwani ameweza kukimbia kwa wastani wa kilomita 7.6.
HAT-TRICK
Cristiano:
Amepiga hat-trick tatu msimu huu, yaani mabao tisa katika mechi tatu. Pia katika mechi moja kati ya hizo tatu alifunga mabao manne peke yake. Mechi alizofunga hat-trick ni dhidi ya Deportivo, Athletic, Celta na Elche.

Messi:
Sasa amefikisha hat-trick nne ikiwa ni moja zaidi ya Ronaldo. Mwanzoni alianza taratibu kabla ya kubadili kasi na sasa anaongoza. Hat trick zake amefunga dhidi ya Espanyol, Deportivo, Levante na Sevilla.

BAO BORA LA LIGA
Cristiano:
Ilikuwa ni bao la kichwa katika mechi dhidi ya Deportivo, ndiyo lilikuwa bao lake bora hadi sasa msimu huu.
Messi:
Alionyesha ana kasi na maamuzi ya haraka, bao lake bora lilipatikana katika mechi dhidi ya Espanyol na likapewa sifa ya ‘best finish’.

0 maoni:

Post a Comment