Na Saleh Ally
TAKRIBANI wiki moja sasa
imepita baada ya Kocha Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic kuvunja ukimya na kusema
kitu ambacho kitakuwa ni mapinduzi makubwa kwenye soka katika klabu hiyo.
Kopunovic, raia wa Serbia,
ameamua kumtaja kiongozi ambaye amekuwa akimpangia timu, kiongozi aliyekuwa
akimlazimisha hata mfumo wa uchezaji anaotakiwa kuutumia!
Kocha huyo Mserbia amemtaja
kiongozi huyo mbele ya viongozi wengine wa Simba, akieleza namna ambavyo
amekuwa akimsisitiza aina ya wachezaji wanaotakiwa kutumika na ambao amekuwa
haamini kama wanatakiwa kucheza katika kikosi cha kwanza.
Achana na kucheza,
Kopunovic alieleza namna kiongozi huyo alivyokuwa akimlazimisha angalau kutumia
mfumo wa 4-4-2 au vinginevyo, kitu ambacho ni cha ajabu kabisa.
Simba na kundi zima la
Friends of Simba (Fos), wamekuwa katika lawama na kashfa muda mrefu, kwamba
wanahusika katika kuwapangia makocha timu wanapokuwa Simba.
Baadhi ya viongozi wa Fos,
wamekuwa wakilikanusha jambo hilo kwa nguvu na kusema makocha wako huru kupanga
wachezaji au kutumia mifumo wanayotaka.
Wamekuwa wakisisitiza
kwamba wao wanaweza kutoa ushauri, hasa wanapoona mambo yanakwenda mlama. Jambo
ambalo linaweza kufanywa hata Ulaya au kwingineko.
Inawezekana kabisa mtindo wa
kuwapangia makocha vikosi au kuwalazimisha watumie mfumo fulani, umekuwa
ukiendelea muda mrefu bila ya wengine kujua.
Nakumbuka wakati Kocha
Patrick Phiri anakaribia kuondoka baada ya Simba kumtupia virago, nilimhoji
kutaka kujua kama alikumbana na tatizo hilo, akakataa katakata.
Sioni ajabu kwa Phiri
kukataa kutokana na namna mwili wake ulivyoumbwa. Mtu mkimya, msiri, asiyependa
kuwaumbua watu na mwenye huruma sana. Kweli binadamu tunatofautiana na Mzambia
huyo ndivyo alivyo.
Pia inawezekana na makocha
kadhaa waliopita hapo awali wapo hivyo, ingawa tuliona Jamhuri Kihwelo ‘Julio’
na Abdallah Kibadeni waliwahi kueleza kero walizokutana nazo, ingawa ilionekana
hatujawaamini sana kwa kuwa ni wazalendo!
Sasa Kopunovic ameweka
mambo hadharani, amekuwa jasiri kutokana na kuona namna kiongozi huyo anavyofanya
mambo ya kizamani, nje ya weledi kumlazimisha au kumuonyesha kazi yake
inafanywa vipi.
Inaonyesha tabia ya
kiongozi huyo haijaanza leo na sasa amejulikana. Ninachohoji, vipi viongozi wa Simba
wanashindwa kumuweka hadharani ili kujisafisha na kashfa hiyo mbaya
iliyowaandama miaka nenda rudi?
Wanasema za mwizi 40, huyu
mtu amepatikana na huu ndiyo ulikuwa wakati mwafaka wa kumuweka hadharani kila
mmoja ajue upuuzi aliokuwa akiufanya.
Kama kiongozi anawapangia
makocha timu, halafu mashabiki wanapiga kelele kulazimisha eti Kocha Msaidizi,
Selemani Matola ndiyo tatizo, basi huu ndiyo wakati mwafaka wa kuweka mambo
hadharani.
Atajwe, kukaa kimya ni
kuficha maradhi ambayo mwisho, Simba wataumbuliwa na kifo. Kiongozi wa namna
hiyo hawafai na wala hapaswi kufichwa.
Pia ningependa kuweka
angalizo, Kopunovic ni kocha na amekuwa wazi, amefanya jambo jema kwa Simba na
soka la Tanzania, sasa asionekane adui na kiongozi huyo kuanza kumpangia njama
za kutaka kuonekana hafai.
Viongozi wote wa soka
wanaofanya kama alivyofanya huyo kiongozi wa Simba hawafai na hawapaswi
kufumbiwa macho kwa kuwa wanachangia kurudisha nyuma mpira wetu.
Kiongozi anayeona anajua
zaidi ya kocha, basi akakae kwenye benchi. Najua akipatikana atasema alikuwa
anatoa maoni, lakini hadi kufikia kocha kusema, hauoni ni tatizo?
Maana yake hata Phiri
alikuwa katika wakati mgumu, huenda alishindwa tu kusema. Bado inaonyesha hata
makocha wengi waliopita walikutana na tatizo kubwa la kiongozi huyo anayejidai
ana uwezo mkubwa kuliko kocha.
Juhudi zimefanyika, lakini
inaonekana Simba wanafanya siri kubwa katika jambo hilo. Hawataki kumtaja,
wanadai wanataka kuvuruga umoja na hata Kopunovic amekuwa hataki kulizungumzia.
Ila siku itafika, Simba
wakiendelea kukaa kimya nitamsaka na kumuweka hadharani ili kukomesha viongozi
kama yeye wenye tabia mbaya na zinazolenga kuumaliza kabisa mpira wa Tanzania
na mwisho yakitokea matatizo, wanaangushiwa makocha kama ilivyokuwa kwa Phiri
au tulivyoona kwa Matola halafu kiongozi husika anakaa kimya na ikiwezekana
anakuwa kati ya wale wanaotangaza kuondolewa kwa kocha. Ujinga kabisa.
0 maoni:
Post a Comment