Feb 22, 2015

CHRISTOPHER ALEX MASSAWE AFARIKI DUNIA



Na Omary Katanga, DAR ES SALAAM
CHAMA cha Soka Dar es Salaam (DRFA), kimeeleza kusikitishwa kwake na kifo cha mchezaji kiungo wa zamani wa klabu ya Simba na timu ya taifa, Taifa Stars, Christopher Alex Masawe, kilichotokea leo (Februari 22, 2015), katika Hospitali ya Mirembe Dodoma.
Mwenyekiti wa DRFA, Almas Kasongo, amemuelezea marehemu Christopher kuwa ni mchezaji aliyevuma enzi za uhai wake na kuiletea heshima kubwa klabu yake ya Simba na Taifa Kwa ujumla, pale walipofanikiwa kuisukumiza nje ya michuano ya afrika klabu ya Zamalek na kuivua ubingwa miamba hiyo ya soka ya kaskazini mwaka 2003.
Christopher Alex Massawe amefariki dunia leo
Christopher Alex Massawe (wa tatu kutoka kulia waliosimama) akiwa na kikosi cha Simba SC mwaka 2003 

Kiungo huyo aliyeanza kuvuma katika miaka ya 2000,amefariki dunia kutokana na kusumbuliwa kwa muda mrefu na ugonjwa wa kifua kikuu (TB).
Marehemu Christopher Alex, alizaliwa Septemba 12 mwaka 1975,na kupata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Uhuru na kumaliza katika shule ya Chamwino huko Dodoma mwaka 1993,na alianza kucheza mpira kwenye timu ya Daraja la nne Chamwino UTD na baadaye daraja la tatu akiwa na kikosi cha Aston Villa nayo ya Dodoma.
Mwaka 1999-2001 ameitumikia klabu ya CDA ya Dodoma,kabla ya kutimkia klabu ya Reli mwaka 2002 na baadaye kujiunga na wekundu wa msimbazi Simba,Marehemu ameacha mtoto mmoja aitwaye Alex.
Kasongo, kwa niaba ya kamati ya utendaji ya DRFA, wametoa ubani wa shilingi laki mbili (200,000/=) kwa familia ya marehemu,na kuwataka mashabiki wa soka na watanzania kwa ujumla kuungana pamoja katika kuifariji familia hiyo kwenye kipindi hiki kigumu cha majonzi.

0 maoni:

Post a Comment