May 4, 2015

KOPUNOVIC; NIMEMALIZA UBISHI, SIMBA NDIYO TIMU BORA TANZANIA, HAKUNA CHA AZAM WALA YANGA


REKODI YA GORAN KOPUNOVIC SIMBA SC

Simba SC 1-0 Mafunzo (Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 1-0 JKU (Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 4-0 Taifa Jang’ombe (Robo Fainali Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 1-0  Polisi (Nusu Fainali Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 0-0  Mtibwa Sugar (Simba ilishinda penalti 4-3 Fainali Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 2-0  Ndanda FC (Ligi Kuu)
Simba SC 1-1 Azam FC (Ligi Kuu)
Simba SC 1-2 Mbeya City (Ligi Kuu Taifa)
Simba SC 2-1 JKT Ruvu (Ligi Kuu)
Simba SC 0-0 Coastal Union (Ligi Kuu)
Simba SC 2-0 Polisi Moro (Ligi Kuu) 
Simba SC 0-1 Stand United (Ligi Kuu)
Simba SC 5-0 Prisons (Ligi Kuu)
Simba SC 1-0 Yanga SC (Ligi Kuu)
Simba SC 1-0 Mtibwa Sugar (Ligi Kuu)
Simba SC 0-2 Mgambo Shooting (Ligi Kuu)
Simba SC 3-0 Ruvu Shooting (Ligi Kuu)
Simba SC 2-1 Kagera Sugar (Ligi Kuu)
Simba SC 3-0 Toto Africans (Kirafiki Mwanza)
Simba SC 0-2 Mbeya City (Ligi Kuu)
Simba SC 4-0 Mgambo JKT (Ligi Kuu)
Simba SC 3-0 Ndanda FC (Ligi Kuu)
Simba SC 2-1 Azam FC (Ligi Kuu) 
Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
KOCHA wa Simba SC, Goran Koponovic amesema kwamba amemaliza ubishi juu ya timu ipi bora kati yao, Yanga na Azam FC.
Kauli ya Mserbia huyo inafuatia jana kuwafunga waliokuwa mabingwa watetezi, Azam FC mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Na kwa kuwa tayari aliwafunga mabingwa wapya, Yanga SC 1-0 katika Ligi Kuu- Kopunovic amesema hiyo inatosha Simba SC kuwa bora zaidi ya wapinzani wake hao.
Alisema licha ya kutotwaa ubingwa, huku akiiombea mabaya Azam ipoteze mechi zake mbili zilizobaki, lakini anajivunia kikosi bora kuliko timu zote za Ligi Kuu Bara. 
“Leo nimemaliza ubishi wa kipi kikosi bora, nimemaliza leo kwamba timu yangu ni bora, hivyo Jumatano nikiwa katika mazoezi akili yangu itakuwa Taifa kwa kuiombea Azam ipoteze mchezo (dhidi ya Yanga) huo ili ipoteze mwelekeo wa nafasi ya pili,'' alisema Goran.
Kocha huyo amesema anaipongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa na pia akawapa pole kwa kutolewa katika Kombe la Shirikisho kufuatia kufungwa 1-0 juzi na Etoile du Sahel nchini Tunisia.
Kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba SC imefikisha pointi 44 baada ya kucheza mechi 25. Azam inabaki na pointi zake 45 za mechi 24 katika nafasi ya pili, wakati tayari Yanga SC imejihakikishia ubingwa baada ya kufikisha pointi 55 za mechi 24.
Simba SC sasa inaiombea dua mbaya Azam FC ipoteze mechi zake zote mbili zilizobaki dhidi ya Yanga na Mgambo- na wenyewe (Simba SC) washinde mechi yao ya mwisho, ili kumaliza katika nafasi ya pili waweze kucheza Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
Tangu atue Msimbazi Januari mwaka huu, Kopunovic ameiongoza Simba SC katika mechi 23 kati ya hizo, imeshinda 17, imefungwa tatu na sare tatu.

0 maoni:

Post a Comment