Feb 6, 2015

KESI YA JAJA KUSIKILIZWA ILALA

Uongozi wa Klabu ya Yanga kupitia kwa Mkurugenzi wa Sheria wa Yanga, Frank Chacha umesema unaendelea kumsubiri mshambuliaji Geilson Santos Santana ‘Jaja’ raia wa Brazil aje nchini kuitikia wito wa kesi waliyomfungulia.

Yanga ilimfungulia kesi mchezaji huyo Mahakama ya Kazi Ilala ambapo imepangwa kusikilizwa Februari 16, ambapo Yanga inadai mchezaji huyo alikiuka vifungu vya sheria wakati alipovunja mkataba wake na timu hiyo.
Wakili Chacha amesema hawatafanya chochote kwa kuwa kisheria mtuhumiwa bado ana nafasi tatu za kuitwa.
“Kwa mujibu wa sheria, ikitokea Jaja hakutokea mahakamani wala kufanya lolote, basi kuna nafasi nyingine tatu za kumwita. Tumeshamtumia e_mail, EMS na kumtumia balozi wake kwa ajili ya kuhakikisha ujumbe wa wito unamfikia kwa wakati ili aweze kuja kusikiliza kesi yake,” alisema.
Yanga iliamua kumfungulia kesi hiyo Jaja aliyejiunga na klabu hiyo Julai 12, 2014 kwa mkataba wa miaka miwili na inamdai faini ya dola milioni mbili (Sh bilioni 3.2), fedha ya usajili dola 20,000 (Sh milioni 32) na dola 3,000 za mshahara wake kwa mwezi mara miezi 12 (jumla Sh milioni 57.6).

0 maoni:

Post a Comment