Feb 6, 2015

KIONGOZI YANGA ALIA NA MAPRO LIGI KUU BARA

TIBODr. Tibohora (kushoto) akiwa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga,Jerry Muro
Na Richard Bakana, Dar es Salaam
KATIBU mkuu wa Mabingwa wa zamani wa ligi kuu ya Soka Tanzania bara, Dar es salaam Young Africans, Dr. Jonas Tibohora, amesema kuwa wachezaji wengi hasa wa kigeni (Professional Players) wameshindwa kutambua thamani yao wakiwa Uwanjani kitu ambacho kinasababisha kushindwa kuwatofautisha na  wazawa.
Akizungumza na Shaffih Dauda.com juu ya matokeo ya kutoridhisha kwa timu kubwa za VPL licha ya kuwa na uwekezaji wa hali ya juu kwenye ligi, Katibu huyo ambaye alichukua mikoba ya Beno Njovu, amesema kuwa inatakiwa iwepo tofauti kubwa kati ya mchezaji wa Kimataifa na mchezaji wa ndani, lakini kutokana na viwango visivyoridhisha kwa wachezaji wa kigeni imekuwa ngumu kutofautisha kati ya timu kubwa na ndogo zinapokutana kwenye mechi za ligi.
Dr. Tibohora amekili kuwa klabu kubwa za Tanzania bara, Simba, Yanga na Azam, zimewekeza sana kwa kununua wachezaji na makocha wa kigeni lakini bado hazioneshi tofauti na timu nyingine zinazotumia makocha na wachezaji wa ndani pekee wanapokuwa Uwanjani.
“Taaluma na maadili ya wachezaji wetu bado inakuwa sio nzuri, Ukiangalia wachezaji wa timu kubwa wanapocheza na timu ndogo unashindwa kutofautisha timu kubwa ni ipi na ndogo ni ipi” Amesema Dr. Tibohora .
Mrundi Amissi Tambwe (kulia) ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni wa Yanga
Timu za Azam FC, Yanga SC, Simba SC ndio timu ambazo zinaongoza kwa kuwa na makocha wa kigeni na wachezaji kutoka nchi za nje lakini matokeo ya Uwanjani hasa zinapokutana na timu kama Ndanda, Stand United na Polisi Morogoro bado unashindwa kutofautisha Kiwango cha wachezaji wa vigogo hao pamoja na hizi timu Changa.
Licha ya kudai kuwa hata uongozi  wa klabu za Tanzania bara zinakosea katika njia za kutafuta na kusajili wachezaji wa kigeni lakini Katibu huyo ametupa zigo la lawama kwa wachezaji wa Kigeni akisema kuwa ni lazima waonyeshe tofauti na thamani yao kama Maprofesional kweli.
Kipre Tchetche ni miongoni wa wachezaji wa kigeni wa Azam fc
“Tatizo ni la wachezaji wetu, Bado hawajaelewa nini maana ya Professionalism, Unapokuwa umepewa kazi lazima ujue  namna gani uwe kama mchezaji wa kulipwa, Ni lazima kuwe na tofauti kati ya mchezaji anayelipwa Milioni tano na yule anayelipwa Laki tatu” Ameongezea Dr. Tibohora.
Kwa upande wake Meneja wa Klabu ya Azam FC, Jemedali Said, amesema kuwa kubweteka kwa wachezaji wa timu kubwa na kukamia kwa timu ndogo ndio kimekuwa sababu ya kufanya utofauti kati ya Simba, Yanga , Ndanda, Ruvu Shooting na Mgambo JKT usionekane pindi wanapokutana katika mchezo.
Jemedali amesema kuwa, Timu ndogo za  VPL zimekuwa na kanuni ya kuzikamia timu kubwa kitu kinachosababisha wachezaji wa timu kubwa washindwe kucheza katika viwango vyao.
Meneja huyo ambaye amewahi kuichezea Yanga amedai kuwa, wachezaji wa timu kubwa wamekuwa na dharau pindi wanapokutana na timu change wakijua muda wowote watapata bao kinyume na wapinzani wao ambao wanakuja kupambana mwanzo mwisho.
“Upinzani uliopo kwa timu hizi tatu kubwa, wachezaji wanaingia Uwanjani wakijua wao ni Nyota, wana viwango vikubwa kitu kinachopelekea washindwe kucheza katika kiwango cha juu, Kwa matokeo yake sasa ukikuta timu ndogo inajituma kwa kiwango kinachotakiwa ndio utaona wanafungwa au kutoa sare” Amesema Jemedali Said Meneja wa Azam FC, huku akiongezea kuwa hata Azam FC kufungwa na Ndanda FC katika ligi ilikuwa ni katika misingi hiyo ya wachezaji kudharau.

0 maoni:

Post a Comment