Mar 7, 2015

JONNY EVANS NAYE ‘JELA’ MECHI SITA ENGLAND

BAADA ya Chama cha Soka England (FA) kumfungia mechi saba mshambuliaji wa Newcastle United, Papiss Cisse kwa kosa la kutemeana mate na beki wa Manchester United, Jonny Evans pia chama hicho kimempa adhabu hiyo beki huyo licha ya kukataa kufanya kosa hilo hapo awali.
FA imemfungia mechi sita kama ilivyotarajiwa, Evans baada ya kuthibitisha tukio hilo katika mkanda wa video wa mchezo huo uliopigwa katika dimba la St.James Park jumatano hii huku Manchester United wakiibuka na ushindi wa 1-0 kwa goli lililofungwa na  Ashely Young katika dakika za majeruhi.

Adhabu hiyo itamfanya beki huyo kukosa mechi ya robo fainali dhidi ya Arsenal itakayopigwa kwenye uwanja wa Old Trafford keshokutwa jumatatu na mechi nyingine atakazokosa ni dhidi ya Tottenham machi 15, Liverpool machi 22, Aston Villa April 4 , Manchester City April 12 na dhidi Chelsea itakayopigwa katika uwanja wa Stamford Bridge April 18.
Aidha kwa upande wa Cisse ambaye amekuwa tegemezi katika klabu ya Newcastle United ameongezewa adhabu ya mechi moja kufuatia na kukutwa na adhabu ya kufungiwa mechi 3 mapema msimu huu kwa kosa la kumchezea vibaya beki wa kulia wa Everton Seamus Coleman.

0 maoni:

Post a Comment