Mar 7, 2015

STURRIDGE ASEMA SASA YUKO 'FULL 100'

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Liverpool, Daniel Sturridge amesema yupo fiti kucheza kila mchezo licha ya kocha wake Brendan Rodgers kumpuzisha katika baadhi ya michezo kwa lengo kumlinda
Baada ya Liverpool kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Burnley katikati ya juma hili kocha Brendan Rodgers alisema amekuwa akimpumzisha mshambuliaji huyo katika baadhi ya mechi ili kumlinda kwani amekuwa akisumbuliwa na majeruhi mara kwa mara.
Sturridge alikaa nje ya uwanja kwa muda miezi mitano mwanzoni mwa msimu huu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya mguu aliyoyapata wakati akiitumikia timu ya taifa ya England.

Hata hivyo mshambuliaji huyo aliyejiunga na majogoo hao mwaka 2013 akitokea klabu ya Chelsea amekuwa moto wa kuotea mbali tangu arejee akitokea majeruhi na kuifanya Liverpool kuvuna pointi nyingi na kushika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi kuu nchini Uingereza.
"Ninajisikia vizuri sana tangu nirudi kutoka majeruhi,na nipo tayari kucheza kila mechi, sitaki niachwe nje lakini inabidi nifuate anachokipanga kocha " alisema Sturridge.
Liverpool ambayo imeshinda michezo minne iliyopita mfululizo katika ligi kuu itashuka dimbani keshokutwa jumapili katika uwanja Anfield kuwavaa Blackburn Rovers ukiwa ni mchezo wa robo fainali katika kombe la FA.

0 maoni:

Post a Comment