Feb 27, 2015

PLUIJM AWAPA UHAKIKA YANGA SC WANALING’OA JESHI LA BOTSWANA AFRIKA

Na Mwandishi Wetu, GABORONE
KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm amewatoa hofu wapenzi wa timu hiyo kuelekea mchezo wa leo dhidi ya BDX XI, akisema kwamba; “tiketi ya kusonga mbele ipo”.  
Yanga SC wanatarajiwa kuwa wageni wa timu hiyo ya Jeshi la Botswana katika mchezo wa marudiano, Raundi ya Awali Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika Uwanja wa Lobetse kuanzia Saa 1:00 usiku kwa saa za huko na Saa 2:00 kwa saa za Afrika Mashariki.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini hapa katika mahojiano maalum kuelekea mchezo wa leo, Pluijm amesema kwamba vijana wake wako tayari kwa kazi nzuri leo. 
Hans van der Pluijm akiwa na Msaidizi wake, Charles Boniface Mkwasa

Kocha huyo ambaye jana asubuhi alifanya mazoezi na kikosi chake katika Uwanja wa Lobetse utakaotumika kwa mcheo huo wa leo, amesema wataingia na akili ya kutaka kuthibitisha ubora wa timu yao.
Pluijm amesema wameuona Uwanja wa mchezo na kwake hauna sababu ya kuifanya timu yake kukosa ushindi na akawaambia wachezaji wake kufanya kweli kwa kupata ushindi lengo likiwa kuthibitisha ubora wa timu yao.
Pluijm amesema wataingia katika mchezo huo kupigana kwa nguvu zao zote ili wapate ushindi mzuri na kusonga mbele.
"Tunataka kuthibitisha ubora wetu kuwa sisi ni Yanga, nimewaambia vijana watulie wacheze kama tulivyokubaliana, kama tutadumisha nidhamu ya mchezo, ushindi upo,"amesema Pluijm.
Yanga SC inahitaji hata sare leo ili kusonga mbele, baada ya awali kushinda mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

0 maoni:

Post a Comment