Mar 11, 2015

SABABU KWA NINI DANNY MRWANDA HAJAINGIA KAMBINI YANGA SC BAADA YA KIPIGO CHA SIMBA JUMAPILI

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
MSHAMBULIAJI Danny Mrwanda hajaingia kambini kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya Platinum ya Zimbabwe, kwa sababu hatacheza siku hiyo, akiwa anatumikia adhabu yake ya kadi nyekundu, Yanga SC imesema.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Mrwanda alipewa kadi nyekundu katika mchezo wa marudiano, Raundi ya Awali Kombe la Shirikisho dhidi ya BDF XI nchini Botswana, hivyo hatacheza Jumapili.
Yanga SC itamenyana na BDF XI Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza, Raundi ya Kwanza Kombe la Shrikisho Afrika na siku hiyo, Mrwanda atakuwa jukwaani.
Danny Mrwanda (kushoto) akitafuta maarifa ya kumtoka Ramadhani Singano 'Messi' (kulia) katika mchezo wa Jumapili

Pamoja na hayo, Muro amesema Mrwanda amepewa ruhusa maalum ya kutokuwa kambini, kwa sababu mke wake ametoka kujifungua.
Kauli hiyo ya Muro- moja kwa moja inazima tetesi kwamba mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba SC amesimamishwa.
Uvumi umekuwa ukiendezwa leo katika kurasa mbalimbali za watu za mitandao ya kijamii, kwamba Mrwanda amesimamishwa kwa sababu alicheza chini ya kiwango Jumapili Yanga ikifungwa 1-0 na mahasimu, Simba SC.
“Huo uzushi wanaoueneza wana nia ya kutuvuruga, lakini sisi kama timu tuko vizuri na wachezaji wetu. Danny ana kadi nyekundu na kila mtu anajua alipewa kadi Botswana, maana yake hatacheza Jumapili. Sasa kwa nini tumlazimishe kuwa kambini?”amesema Muro.
Mrwanda aliikosesha Yanga SC bao la wazi dakika ya 28 siku hiyo, baada ya kupewa pasi nzuri na Simon Msuva, lakini akazubaa na mpira ndani ya boksi hadi akapokonywa na Juuko Murushid.
Tukio hilo lilimkera kocha Mholanzi wa Yanga SC, Hans van der Pluijm ambaye alimtoa mchezaji huyo dakika mbili baadaye na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Javu na kipindi cha pili, Emmanuel Okwi akaifungia bao pekee Simba SC la ushindi katika mchezo huo wa Ligi Kuu.

0 maoni:

Post a Comment