Mar 11, 2015

VAN GAAL ‘AMPA MAKAVU’ DI MARIA, ASEMA ALIIPONZA TIMU KUFUNGWA NA ARSENAL

KOCHA wa klabu ya Manchester United, Louis Van Gaal amemponda winga wake Angel Di Maria kwa kosa la kupata kadi nyekundu katika mchezo wa jana wa robo fainali kombe la FA dhidi ya washika bunduki Arsenal uliopigwa katika dimba la Old Trafford.
Winga huyo aliyevunja rekodi ya usajili nchini Uingereza alipata kadi nyekundu baada ya kupewa kadi ya njano ya pili kwa kumsukuma mwamuzi Michael Oliver huku akiwa na kadi ya njano ambayo aliipata muda huo huo kwa kosa la kujiangusha baada ya kukabwa na kiungo wa Arsenal, Aaron Ramsey.

Van Gaal alisema mchezaji huyo alikosa umakini mpaka akapata kadi hiyo ambayo ilipelekea kuongeza ugumu wa mchezo na kufanya Arsenal kuongeza kasi ya mashambulizi langoni kwa mashetani hao.
"Di Maria anajua kuwa mchezaji haruhusiwi kumshika mwamuzi lakini hakulijali hilo.Alikosa umakini katika hilo kwani nilizingumza kabla ya mchezo kwamba kupata kadi nyekundu katika mechi kama hii ni rahisi sana ila hajazingatia hilo. " alisema Van Gaal.
Pia kocha huyo amesema alisikitishwa na kiwango kilichooneshwa na timu yake katika mchezo huo na sasa nguvu zote anazielekeza katika kuwania nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa msimu ujao.
Katika mechi hiyo ya robo fainali Arsenal iliibuka na ushindi wa 2-1, magoli ya Arsenal yakifungwa na Nacho Monreal na Danny Welbeck huku la Mashetani hao likifungwa na nahodha wao Wayne Rooney.
Hii ni mara ya kwanza kwa washika bunduki hao wa jiji la London kuifunga Manchester United katika uwanja wa Old Trafford tangu wafanye hivyo mwaka 2006.
Baada ya kutinga hatua ya nusu fainali Arsenal watacheza na mshindi kati ya Bradford City na Reading ambao wanataraji kucheza mechi yao ya marudiano jumatatu ijayo baada ya kutoka sare ya 0-0 katika mechi ya kwanza.


0 maoni:

Post a Comment