Feb 5, 2015

ALICHOSEMA KOCHA AZAM BAADA YA KUMALIZA ZIARA DR CONGO


 
KOCHA Mkuu wa Azam FC, Mcameroon Joseph Marius Omog (pichani kushoto) amesema ziara ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ilikuwa ya mafanikio. 
 
Akizungumza jana jioni baada ya kurejea Dar es Salaam, Omog alisema kwamba japokuwa hawajashinda mechi, lakini wamepata faida kubwa katika michezo mitatu waliyocheza.
“Tulikuja huku kwa ajili ya kujifunza na tumecheza dhidi ya timu za kiwango cha juu, kilikuwa ni kipimo tosha cha tunavyoweza kucheza na mpinzani mgumu ugenini. Dhamira yetu imetimia,”amesema Omog.
 
Mcameroon huyo amesema sasa vijana wake wapo tayari kwa mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Merreikh ya Sudan wiki ijayo, baada ya mazoezi mazuri DRC.  
Azam FC juzi ilihitimisha ziara yake ya Lubumbashi, DRC bila ya ushindi baada ya kufungwa bao 1-0 Don Bosco ya Kinshasa Uwanja wa TP Mazembe mjini humo.
 
Awali, mabingwa hao wa Tanzania Bara, walilazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na ZESCO United ya Zambia mabao yake yakifungwa na kiungo Frank Domayo. Mchezo wa kwanza, Azam FC walifungwa 1-0 na wenyeji wao, TP Mazembe.
 
Baada ya kurejea Dar es Salaam jana, Azam FC watakuwa kambini kwao, Azam Complex, Chamazi hadi Jumamosi watakaposafiri kwenda Morogoro kumenyana na Polisi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Wakitoka Morogoro, Azam FC watarejea nyumbani kucheza mechi nyingine ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar na baada ya hapo wataingia kwenye maandalizi ya mwisho kwa ajili ya BDF.  

0 maoni:

Post a Comment