Feb 5, 2015

TUMBA SWEDI BEKI MZURI INGAWA HAITWI STARS

BEKI wa Coastal Union, Tumba Swedi ‘Mdudu Kiwi’ jana alinusurika kupewa kadi nyekundu timu yake ikimenyana na Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. 

Tumba, alimchezea rafu mshambuliaji wa Yanga SC, Kpah Sherman kipindi cha pili na refa Athumani Lazi wa Morogoro akapiga filimbi mpira utengwe upigwe kuelekezwa lango la Coastal.
Lazi hakuwa na dhamira ya kumpa kadi yoyote Tumba, kwa sababu ilikuwa faulo ya kawaida ya kumzibia njia Mliberia wa Yanga. Hata hivyo, pamoja na kutambua amefanya kosa kimchezo, lakini Tumba alimjia juu refa na kumtolea maneno makali.
Tumba akimtolea maneno makali refa Athumani Lazi jana Uwanja wa Mkwakwani
Tumba akionyeshwa kadi ya njano na Lazi
Faulo iliyosababisha yote hayo ni hii hapa

 
Lazi akamuita Tumba kwa ajili ya kumpa kadi, ambayo wazi ingekuwa ya njano, lakini beki huyo akaendelea kumfanyia ukaidi mwamuzi huyo, huku akimtolea maneno makali.
Ajabu, Lazi alikuwa mpole wakati akifokewa na beki huyo aliyeibukia akademi ya Azam FC, kabla ya kutolewa kwa mkopo Moro United, baadaye Ashanti United na sasa yupo katika msimu wake wa kwanza Coastal.
 
Refa huyo alikuwa ameweka mikono yake nyuma huku akimsikiliza kijana huyo akitoa maneno yake na kurusha mikono kama anayetaka kumuadhibu mwamuzi huyo.
Tukio hilo liliwafanya mashabiki wa Coastal wanyamaze kimya, wakihofia kinachofuatia kwa mchezaji huyo ni kadi nyekundu.
 
Lakini bahati nzuri iliyoje, baada ya vurugu zote Lazi alimpa kadi ya njano tu mchezaji huyo. Hata hivyo, Tumba alirudia kumtolea maneno makali refa huyo baada ya kadi kuashiria kwamba hakujali adhabu hiyo.
Inawezekana kabisa ikawa ni hasira iliyotokana na upinzani wa mchezo huo, lakini ukweli ni kwamba hakuna ambaye angeshangaa kama Lazi angemuonyesha kadi nyekundu beki huyo.
 
Matukio kama haya wamekuwa wakifanya wachezaji wengi katika soka ya Tanzania, lakini bahati mbaya ni kama makocha wao hawawakemei na ndiyo maana wamekuwa wakirudia.
Pamoja na kufundisha, kuongoza mazoezi, walimu wanapaswa kujua wana wajibu pia wa kuwafundisha nidhamu ya mchezo wachezaji wao. Wana wajibu wa kuwandaa kuwa wachezaji kamili katika soko.
 
Mchezaji kama Tumba, ni ambaye ameibukia kwenye mfereji mzuri kisoka, akianzia shule, akademi ya Azam FC ambako alikaribia kupandishwa kikosi cha kwanza chini ya kocha Muingereza Stewart Hall.
Walichoshindwana Tumba na Hall ni juu ya nafasi ya kucheza, kocha Muingereza akitaka kumuhamishia beki ya pembeni, kitu ambacho mchezaji huyo hakutaka na akaamua kuondoka.
 
Lakini Tumba akawa tegemeo la timu za vijana za taifa kuanzia U17 na baadaye U20, ingawa baada ya kutua Ashanti amepoteza bahati ya kuitwa timu za taifa.
Hakuna shaka kuhusu uwezo wa Tumba, ni beki ‘ngangali’, mwenye maarifa na uwezo wa hali ya juu. Anapiga mashuti ya mbali na kufunga na kwa ujumla ni mzuri hata kwenye kusaidia mashambulizi wakati wa mipira ya kona anaweza kufunga hadi kwa kichwa.
 
Lakini kitu kimoja tu, Tumba anapaswa kuangalia nidhamu yake mchezoni, inawezekana kwa namna moja au nyingine, inampunguzia mambo fulani fulani bila yeye mweneywe kujua.
Kwa mfano kwa sasa, pamoja na ubora wake amefungiwa vioo timu za taifa, inawezekana labda kwa tabia zake kama hizi walimu wanaamua kumchunia. 

0 maoni:

Post a Comment