Feb 5, 2015

KISIGA ATOA YA MOYONI SIMBA, AWATAJA AMBAO WANAKALIBIA KUACHWA

SHABAN Kisiga amelitumia Mwanaspoti kuwaeleza mashabiki zaidi ya milioni 20 wa Simba ukweli wake wa rohoni wa nini hasa kinachoendelea na kilichomtoa kwenye timu hiyo.
Hata hivyo, alichosisitiza zaidi ni kwamba ilikuwa inamdhalilisha kwa kumkalisha benchi ila Mwanaspoti limepata habari za uhakika kutoka ndani kwamba kuna wachezaji wawili wakongwe nao watamfuata kiungo huyo.


Wachezaji hao ni kipa Ivo Mapunda (pichani) ambaye ndiye mchezaji pekee wa Simba aliyewahi kuwa askari akaacha kazi na beki Nasoro Masoud ‘Chollo’ ambao hata hivyo mikataba yao itamalizika mwishoni mwa msimu, huku Awadh Juma, Elius Maguri na Jonas Mkude wanadaiwa kuwa na nidhamu mbovu na wanachunguzwa kimya kimya.

Kisiga ambaye anaishi Yombo jijini Dar es Salaam, aliliambia Mwanaspoti kuwa alikuwa akivumilia hali hiyo kwa kuamini kwamba mambo yangebadilika, lakini haikuwa hivyo hata pale alipokuja kocha mpya Mserbia Goran Kopunovic ambaye aliendelea kumwingiza akianzia benchi.
Alisema anaamini kama Kopunovic (48), angekuwa ameachwa huru kupanga kikosi huenda angekuwa anapewa nafasi ya kucheza.

“Niliamua kuondoka kwa sababu niliona nadhalilika sana na kwa nini nifikie hatua hiyo? Mimi si mchezaji wa kupewa dakika 10 au tano kucheza, inaumiza sana hasa pale unapojua ni kwa nini hupangwi, yote haya yalikuwa yanatokea kwa chuki ya mtu jambo ambalo mimi huwa sikubaliani nalo,” alisema Kisiga ambaye amewahi kuichezea SC Villa ya Uganda.

“Hivyo ni vyema niondoke ili niwaachie wengine ambao wana nafasi ya kucheza kuliko kwenda kambini unakula na kulala bure halafu huchezi, najua hawaumii juu yangu kwani hata usajili wangu ni wa kawaida sana ukilinganisha na wachezaji wao waliowasajili kwa mamilioni ya fedha, lakini mimi nazingatia heshima yangu.”
Kiungo huyo mtaalamu wa kupiga faulo, alisema kuwa inasikitisha kuona mpira wa Tanzania kwa sasa unaendeshwa kwa fitina na si kuzingatia uwezo wa mchezaji husika ukoje.
“Najua hata kocha alipotua tu Zanzibar aliambiwa watu wa kuanza kuwapanga na wale wa kuanzia benchi, hizo ni fitina mbaya ambazo zinaua viwango vya wachezaji wengi hapa nchini, mpira hautaki majungu, uwezo wa mtu unaonekana uwanjani.

0 maoni:

Post a Comment