MCHEZAJI wa Azam, Erasto Nyoni, amekuwa akicheza nafasi kadhaa kikosini humo na pia timu ya taifa,
Taifa Stars. Unamjua aliyempa uwezo huo ni nani? Amefichua kuwa ni kocha Marcio Maximo, aliyemhamisha kutoka kiungo na kuwa beki.
Nyoni alisema wakati Maximo anaifundisha Taifa
Stars kati ya mwaka 2006 na 2010, ndipo alipobadilishwa nafasi kutoka
kiungo mkabaji na kupelekwa kucheza beki wa pembeni.
Mchezaji Bora huyo wa Tuzo za Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (Taswa) mwaka jana, amekuwa akicheza beki wa kulia, kushoto, kati na pia kiungo jambo ambalo ni nadra kwa wachezaji wengine.
“Naweza kucheza beki wa pembeni kwa pande zote
mbili, pia huwa nacheza beki wa kati na wakati mwingine nacheza kiungo
na ninamudu nafasi zote hizo vizuri bila ya wasiwasi,” alisema.
“Maximo ndiye alinibadilisha wakati anaifundisha timu ya Taifa, mwanzoni nilikuwa nacheza kiungo mkabaji na sikuwahi kucheza beki,” alisema Nyoni.
Katika hatua nyingine, kocha wa Don Bosco, Kasongo
Ngandu, amesema kikosi cha Azam kinacheza vizuri lakini umaliziaji wao
ni mbovu jambo ambalo litaigharimu timu hiyo katika mechi kubwa.
Azam ilifungwa bao 1-0 na Don Bosco juzi Jumanne ikiwa ni mechi yake ya mwisho mjini hapa. Kikosi cha Azam kilirejea Dar es Salaam jana kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Morogoro.
Ngandu alisema: “Timu yao ni nzuri lakini ina tatizo katika ufungaji, umaliziaji wao siyo mzuri.
“Viungo wao wanatakiwa kucheza kwa kushambulia zaidi kuliko wanavyocheza sasa, wakiweza kurekebisha itakuwa bora kwao.”
0 maoni:
Post a Comment