Feb 9, 2015

MAGWIJI WA BARCELONA KUKIPIGA DAR

KIKOSI cha magwiji wa Barcelona kitazuru Dar es Salaa Machi 28 mwaka huu kwa ajili ya mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya wachezaji nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, maarufu Tanzania Eleven.
Almasi Kasongo, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Dar es Salaam, wanaoandaa ziara hiyo kwa ushirikiano na kampuni ya Prime Time Promotions amesema hayo leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari ukumbi wa City Sports Lounge, Dar es Salaam.
 
Mkutano huo, ulihudhuriwa na mkali wa zamani wa mabao wa Barcelona, Mholanzi Patrick Kluviert ambaye amethibitisha ujio wa nyota waliotaka Camp Nou miaka ya nyuma kidogo.
Ziara hiyo ni matunda ya ziara ya magwiji wa wapinzani wa Barcelona, Real Madrid Agosti mwaka jana, ambao pia walicheza na magwiji wa Tanzania na kushinda 3-1 Dar es Salaam.
Patrick Kluivert katikati akizungumza na Waandishi wa Habari Dar es Salaam leo

Mchezo huo, uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Agosti 23, mwaka jana na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Reuben de La Red alifunga mabao matatu peke yake, magwiji.
 
De la Red alimfunga bao moja Mwameja Mohamed kipindi cha kwanza na kipindi cha pil akamtungua mara mbili Manyika Peter, wakati bao pekee la Stars, Real walijifunga wenyewe kupitia kwa Roberto Rojas.
Siku hiyo, Rais Kikwete alimkabidhi mpira De La Red baada ya mechi kabla ya kuwakabidhi Kombe Real Madird kwa ushindi huo.
 
Katika mchezo huo, ambao wachezaji waliingia na kutoka, Real Madird walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 10, De La Red akimalizia pasi ya Luis Figo.
Mpira uliozaa bao hilo, ulianzia kwa kiungo Christian Karembeu, aliyezuia shambulizi la Tanzania na kuanzisha shambuizi zuri lililozaa matunda, akiuvuka msitu wa wachezaji wa wenyeji kwa umahiri mkubwa.
 
Tanzania Eleven ilisawazisha dakika ya 45 baada ya kona ya Mecky Mexime kuzua kizaa langoni mwa Real na Roberto Rojas akajifunga katika harakati za kuokoa baada ya Kali Ongala kuuparaza kwa kichwa. 
Kipindi cha pili, De la Red alifunga bao kwa pili kwa penalti dakika ya 81 baada ya yeye mwenyewe kuchezewa rafu na Habib Kondo kwenye eneo la hatari.
Awali ya hapo, Figo alimtoka vizuri beki Mecky Mexime na kuingia hadi kwenye eneo la hatari akiwa 

kwenye nafasi ya kufunga akampasia De La Red ambaye alipiga nje.
De la Red alikamilisha hat trick yake dakika ya 88 baada ya kuwazidi maarifa mabeki wa Tanzania Eeleven na baada ya hapo, wachezaji wa timu zote mbili wakajumuika katika hafla ya chakula cha usiku na Mheshimiwa Rais Ikulu.

0 maoni:

Post a Comment