Mshambuliaji nyota wa Simba, raia wa Uganda,
Emmanuel Okwi, anadaiwa kubadili mfumo wake wa maisha ndani ya klabu hiyo tangu
aliporejea kutoka katika likizo ya ndoa aliyokuwa amepewa na uongozi wa timu
hiyo baada ya kuoa.
Okwi ambaye hapo awali alikuwa akidaiwa kuwa
na tabia ya usumbufu, hivi sasa ni mtoto mwema kutokana na kuwa msitari wa
mbele kuzingatia kila jambo analoagizwa kufanya na kocha mkuu wa timu hiyo, Mserbia,
Goran Kopunovic.
Hali hiyo, Pia imewafanya viongozi wa timu
hiyo kutoyaamini macho yao kwani walizoea kumwona akiwa tofauti kabisa na
alivyo hivi sasa ikiwa ni baada ya kuoa.
Kopunovic ambaye amejiunga na Simba akichukua
mikoba ya Mzambia, Patrick Phiri, alisema kuwa kila siku zinavyozidi kusonga
mbele ndivyo Okwi anavyozidi kubadilika kwani tabia yake ya sasa ni ya kuigwa
na wachezaji wote katika kikosi hicho.
“Hakika najivunia kuwa na mchezaji kama Okwi
katika kikosi changu kwani ni mfano wa kuigwa na wenzake kuanzia ndani na nje
ya uwanja, japokuwa hapo awali nilisikia kuwa ni msumbufu lakini binafsi
usumbufu huo sijauona.
“Hata hivyo nimekuwa nikisikia baadhi ya
wachezaji wenzake wakimtania kuwa tangu alipooa amebadilika sana, labda hiyo
ndiyo sababu,” alisema Kopunovic.
0 maoni:
Post a Comment