Mar 14, 2015

MARSH KUAGWA JUMATATU KARUME, MAZISHI MWANZA

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
MWILI wa aliyekuwa kocha Msaidizi wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Sylvester Marsh utaagwa Jumatatu kuanzia Saa 4:00 asubuhi Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa Mwanza kwa mazishi.
Mtoto wa kaka wa marehemu Marsh, aitwaye Abdallah Ramadhani, ambaye alikuwa anamuuguza baba yake mdogo amesema taratibu za mazishi zinaendelea.  
Marsh amefariki dunia Alfajiri ya leo katika hospitali ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya saratani ya koo.
Na ilielezwa, Marsh alikuwa amekuja Muhimbili kuhudhuria kliniki yake ya kawaida juu ya maradhi ya saratani ya koo yanayomsumbua na ghafla hali yake ikabadilika juzi hadi kufariki dunia.
Sylvester Marsh (katikati) enzi za uhai wake akiwa Jacob MIchelsen kulia na Kim Poulsen kushoto

Marsh alianza kuwa Kocha Msaidizi wa timu za vijana Tanzania mwaka 2003 chini ya Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ kabla ya mwaka 2006 kupandishwa timu ya wakubwa, akianza kumsaidia Mbrazil, Marcio Maximo na baadaye Wadenmark, Jan Poulsen na Kim Poulsen.
Hata hivyo, baada ya Jamal Malinzi kushinda Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Oktoba mwaka juzi, alibadilisha benchi zima la ufundi la Taifa Stars na Marsh akaondoka pamoja na Kim Poulsen. Sasa Mholanzi, Mart Nooij ndiye kocha Stars, anasaidiwa na Salum Mayanga.
Tangu hapo Marsh amerudi kufanya kazi katika kituo chake cha Marsh Academy mjini Mwanza, lakini mwaka jana ndipo maradhi ya saratani koo yalipoibuka na akaletwa Muhimbili kwa matibabu.
Mfanyabiashara Abdulfatah Salim, mmiliki wa hoteli ya Sapphire Court, alimsaidia kocha huyo hadi akafanyiwa upasuaji na hali yake kuimarika Februari mwaka jana na kurejea Mwanza.
Marsh alipata ahueni ya kutosha na kuanza tena kazi ya kufundisha watoto wake wa Marsh Academy, kabla ya wiki hii kuletwa Dar es Salaam kuhudhuria kliniki.
Mbali na timu za taifa, Marsh pia amefundisha klabu za Toto Africans ya Mwanza, Kagera Sugar ya Bukoba na Azam FC ya Dar es Salaam.
Miongoni mwa mafanikio yake akiwa kocha, mwaka 2005 aliiwezesha Kagera Sugar kutwaa Kombe la Tusker, ikiifunga Simba SC katika fainali mabao 2-1 Dar es Salaam.
Mwaka 2004, akiwa Msaidizi wa Kibadeni katika U17, maarufu Serengeti Boys, waliiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza Fainali za Afrika nchini Gambia, baada ya kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe. 
Hata hivyo, timu hiyo iliyoibua vipaji vya wachezaji waliogeuka nyota wa taifa kwa miaka 10 iliyopita kama Nizar Khalfan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Amir Maftah na wengine, ilienguliwa fainali za Gambia kwa kashfa ya kumtumia Nurdin Bakari aliyekuwa amezidi umri.
Mwaka 2009, Marsh akiwa Msaidizi wa Maximo Taifa Stars, waliiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza fainali za kwanza za CHAN nchini Ivory Coast.
Inaelezwa kwa muda wote wa Marsh kufanya kazi na timu za taifa hakuwahi kuwa na Mkataba, bali alikuwa kama ‘deiwaka’ maana yake hakuweka mbele maslahi, bali uzalendo. 
Bwana ametoa, bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe. Mbele yake, nyuma yetu. Mungu ampumzishe kwa amani mwalimu Sylvester Marsh. Amina. 

0 maoni:

Post a Comment