Mar 14, 2015

WAKURUGENZI AZAM FC WAPATA ‘LANCHI’ NA WACHEZAJI, WAPANGA NAO MIKAKATI YA KUTETEA UBINGWA

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
WAKURUGENZI wa klabu ya Azam FC, leo wamesali pamoja na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo sala ya Ijumaa kabla ya kupata nao chakula cha mchana wachezaji wote.
Hiyo ilikuwa kabla ya kikao maalum cha kuweka mikakati ya kuhakikisha timu inatetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kilichofanyika Mikocheni, Dar es Salaam, nyumbani kwa Yussuf Bakhresa, mmoja wa Wakurugenzi.
Pamoja na Yussuf, alikuwepo Omar Bakhresa, wote watoto wa bilionea Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa, na mdogo wake, Jamal Bakhresa.
Yussuf Bakhresa akizungumza na wachezaji leo nyumbani kwake, Mikocheni, Dar es Salaam
Jamal Bakhresa kulia na Omar Bakhresa kushoto wakichukua chakula
Katibu wa Azam FC, Nassor Idrisa 'Father' kulia akiwa na Omar Bakhresa 

Wakurugenzi hao walianza kwa kuwapongeza wachezaji kwa kuifikisha timu ilipo sasa na wakawaambia hawajasononeshwa na kutolewa kwao katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Azam FC ilitolewa na El Merreikh ya Sudan katika Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikifungwa 3-0 ugenini baada ya kushinda 2-0 nyumbani.
Baada ya hapo, uongozi ulimfukuza kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog na msaidizi wake namba mbili, Mkenya Ibrahim Shikanda na timu kwa sasa ipo chini ya Mganda, George ‘Best’ Nsimbe.
Juzi, bodi ya Ukurugenzi imemuongeza aliyekuwa kocha wa Ndanda FC, Dennis Kitambi kuwa Msaidizi wa Nsimbe kwa muda.
Katika kikao hicho, Omar Bakhresa aliwaambia wachezaji kwamba wao hawajasononeshwa na matokeo ya timu kutolewa mapema Ligi ya Mabingwa kwa sababu wanafahamu hiyo ndiyo soka.
“Timu kama Manchester City, inawekeza fedha nyingi mno, inasajili wachezaji wakubwa duniani, lakini bado haijaweza kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Ulaya,”.
“Sasa na sisi tunajua ni suala la wakati tu, wakati ukifika Azam itakuwa bingwa wa Afrika, hizo ndizo ndoto zetu na ndiyo maana hatuchoki kuwekeza kila siku,”alisema.
Yussuf Bakhresa kwa upande wake aliwaambia kwamba wachezaji hawatakiwi kujisikia unyonge kwa kutolewa mapema kwa sababu hayo ni matokeo ya kawaida katika soka.
“Sisi tuliona, mlipambana kadiri ya uwezo wenu. Kwanza tunawapongeza hata kuwafunga 2-0 hapa nyumbani, halikuwa jambo jepesi. Tunaomba msife moyo, huo si mwisho. Jitahidini mtetee ubingwa wa Ligi Kuu, ili mwakani muende mkasahihishe makosa yenu,”alisema.
Yussuf amewataka wachezaji wao kwa wao kushikamana, kupendana na kucheza kwa ari kuhakikisha wanachukua tena ubingwa wa Ligi Kuu.
“Yanga wanatuzidi pointi moja. Hii maana yake tunapaswa kushinda mechi zetu zote zilizobaki ikiwemo mechi yetu dhidi yao, ili tuwe mabingwa. Hii si kazi nyepesi, lakini kwa sababu tunaamini uwezo wenu, tunaamini inawezekana,”alisema Yussuf.
Yussuf aliwaambia nia ya Bodi ya Ukurugenzi ipo pale pale, ni kuifanya Azam FC iwe klabu kubwa Afrika na mikakati zaidi ya kuboresha mfumo wa uendeshwaji inakuja.
“Siku si nyingi, mtasikia mambo makubwa sana hapa Azam, itakuwa klabu ya kipekee Afrika. Sitaki kuwaambieni kila kitu, ila vuteni subira mtasikia,”alisema.
Naye Jamal Bakhresa, aliwaambia wachezaji waongeze juhudi kwa sababu sasa ushindani ni mkubwa katika Ligi Kuu.
Wachezaji wa Azam FC wakichukua chakula nyumbani kwa bosi wao jana
Jamal Bakhresa (kushoto) akizungumza huku Yussuf Bakhresa (kulia) na Kipre Tchetche (katikati) wakisikiliza
Wachezaji wa Azam FC, Gaudence Mwaikimba kulia na Erasto Nyoni kushoto jana kwa 'bosi Yussuf' mchana

“Simba SC wanakuja, wapo nyuma yetu. Nao wanataka nafasi. Kwa hiyo mnatakiwa kucheza kila mechi kama fainali, ligi ipo ukingoni hii. Sasa hivi kila timu itawakamieni, lakini ni wanaume wenzetu hao, pambaneni na muwafunge,”alisema. 
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, Nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliwashukuru Wakurugenzi kwa kuonyesha wanawajali na akaahidi wanakwenda kupambana kuhakikisha wanatetea ubingwa.
“Sisi tunashukuru sana, hii mmeonyesha mnatujali na nyinyi ni watu wa michezo kweli. Kweli tulisikitishwa baada ya kutolewa na El Marreikh, kwa sababu dhamira yetu ilikuwa ni kufika mbali,”
“Lakini tunasema hayo yote tunayaacha nyuma, na sasa tunaelekeza nguvu katika kutetea ubingwa,”alisema Bocco.   
Kwa sasa katika msimamo wa Ligi Kuu, Azam FC inashika nafasi ya pili kwa pointi zake 30, nyuma ya Yanga SC, yenye pointi 31, baada ya kila timu kucheza mechi 16. Simba SC yenye pointi 26 ni ya tatu baada ya kucheza mechi 17.
Wakati Azam FC itashuka tena dimbani Jumatatu kumenyana na Ndanda FC, Simba SC wao watamenyana na Mtibwa Sugar kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga SC keshokutwa itameyana na Platinum FC ya Zimbabwe katika mchezo wa kwanza, Raundi ya Kwanza, Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya katikati ya wiki kukipiga na JKT Ruvu katika Ligi Kuu.    

0 maoni:

Post a Comment