Mar 14, 2015

MIKATABA YA NIYONZIMA, NGASSA YAMALIZIKA YANGA, WAKO HURU KWENDA ZAO

NGASSA (KULIA....
Viungo wa Yanga Mnyarwanda, Haruna Niyonzima na Mrisho Ngassa wamesema, mikataba yao imekwisha na wanawaaga kabisa mashabiki wao.

Viungo hao, kila mmoja ameaga kuondoka kwa sababu tofauti huku ikikumbukwa kuwa mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Kauli hiyo, imetolewa na viungo hao ikiwa ni siku chache tangu kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba ambayo ilimalizika kwa Yanga kufungwa bao 1-0 kabla ya tuhuma za hujuma kwa wachezaji wa timu hiyo kutolewa na mashabiki.
Niyonzima amesema kuwa imetosha kuichezea Yanga, hivyo ameona bora aondoke na kuwaachia mashabiki timu yao huku akiitakia mafanikio.
 
NIYONZIMA (KULIA)...
Niyonzima alisema, kichwa chake hakipo vizuri, hivyo anahitaji muda zaidi wa kupumzisha akili yake kwa kutoongeza mkataba mwingine na kurudi kwao Rwanda.
Mrwanda huyo alisema amechoshwa na kashfa anazoendelea kupewa na baadhi ya viongozi na mashabiki wa Yanga kuhusiana na kuihujumu kwenye mechi dhidi ya Simba.
“Nilikuwa tayari kuongeza mkataba mwingine wa kuichezea Yanga baada ya hivi karibuni kufanya mazungumzo na viongozi, lakini nimesitisha mpango huo hivi sasa na badala yake nitarudi zangu nyumbani kupumzika.
“Kiukweli nimechoshwa na taarifa za mimi kila tunapokutana na Simba ninacheza chini ya kiwango, mechi ya mwisho tuliyocheza na Simba wiki iliyopita mengi yaliongelewa na baadhi ya viongozi na mashabiki kuwa nimeihujumu timu kwa kucheza chini ya kiwango, kitu ambacho siyo kweli.
“Hivyo sitasaini tena Yanga na badala yake nitarudi zangu Rwanda kupumzisha akili yangu, pia sipo tayari kuichezea timu yoyote ya hapa nchini, kwa sababu matatizo yaliyopo Yanga yapo huko pia,” alisema Niyonzima.
Kwa upande wa Ngassa yeye alisema: “Mimi sasa hivi akili yangu inafikiria kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na siyo hapa nchini, zipo tetesi nyingi zinazozungumza kuwa nimesaini Simba mara Azam FC.


“Ukweli ni kwamba hiki ndiyo kipindi changu muafaka kwa mimi kuondoka Yanga, ninataka mafanikio zaidi, ninaondoka Yanga bila ya kinyongo na mtu, niliipenda timu yangu ya Yanga lakini sitarajii kuongeza mkataba,” alisema Ngassa.

SOURCE: CHAMPIONI JUMAMOSI

0 maoni:

Post a Comment